15. Sura ya nne: Dalili ya tatu inayothibitisha juu ya upwekekaji wa Allaah katika uumbaji, riziki na mengineyo III


3- Kudhalilishwa kwa viumbe katika kutekeleza kazi zao na kusimamia mambo yao yanayowahusu. Hakuna kiumbe yeyote atakayefanya ukaidi na kukataa kutekeleza kile anachokitaka Allaah katika ulimwengu huu. Haya ni miongoni mwa yale aliyotumia dalili Muusa (´alayhis-Salaam) wakati Muusa alipomuuliza:

فَمَن رَّبُّكُمَا يَا مُوسَىٰ

”Basi ni nani Mola wenu, ee Muusa?”

Muusa akajibu kwa jibu linalotosha na linalokata kiu kwa kusema:

رَبُّنَا الَّذِي أَعْطَىٰ كُلَّ شَيْءٍ خَلْقَهُ ثُمَّ هَدَىٰ

”Mola wetu ni Yule aliyekipa kila kitu umbo lake kisha akakiongoza.”[1]

Bi maana Mola wetu ni yule ambaye amewaumba viumbe wote na akakipa kila kiumbe umbile linaloendana naye katika ukubwa wa mwili, udogo wake, ukatikati wake na sifa zake zote. Akamwongoza kila kiumbe katika kile alichoumbiwa. Uongofu huu ni uongofu wa maelekezo na ni uongofu kamilifu unaoshuhudiwa katika viumbe wote. Kila kiumbe utamwona ni mwenye kupupia katika yale manufaa aliyoumbiwa na katika kujizuia na madhara kwake. Kiasi cha kwamba Allaah amewapa mpaka wanyama fahamu fulani inayowawezesha kufanya yenye kuwanufaisha, kujiepusha na yanayowadhuru na yenye kuwafanya wakaweza kutimiza mambo yao ya kila siku katika maisha yao. Haya ni kama maneno Yake (Ta´ala):

الَّذِي أَحْسَنَ كُلَّ شَيْءٍ خَلَقَهُ

“Ambaye amekifanya uzuri kila kitu alichokiumba.”[2]

Ambaye ameviumba viumbe wote na akavipa umbile zuri – ambalo hakuna akili iwezayo kufikiria zaidi ya uzuri  wake – na akaviongoza katika manufaa yake. Huyu ndiye Mola wa kweli. Kumpinga ni kupinga kitu kikubwa kilichopo, jambo ambalo ni jeuri na kudhihirisha uongo. Allaah amewapa viumbe kila kitu wanachokihitajia duniani kisha akawaongoza katika njia ya kunufaika navyo. Hapana shaka kwamba kila aina ya kiumbe amekipa shakili yake na sura yake inayonasibiana nacho. Vilevile amempa kila mume na mke shakili yake inayonasibiana na aina yake katika kuoana, muungamano na kukusanyika. Isitoshe kila kiungo amekipa muundo wake unayolingana na manufaa yake. Katika haya kuna dalili zenye kukata kabisa juu ya kwamba Yeye (Jalla wa ´Alaa) ni Mola wa kila kitu. Yeye ndiye anastahiki ´ibaadah pasi na mwengine.

Katika kila kitu kuna alama

inayothibitisha kuwa Yeye ni Mmoja

Miongoni mwa mambo yasiyokuwa na shaka yoyote ndani yake ni kwamba malengo ya kuthibitisha uola Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) juu ya viumbe Wake na kupwekeka Kwake juu ya hayo ni kutumia dalili kwa hayo juu ya ulazima wa kumwabudu Yeye pekee, hali ya kuwa peke yake hana mshirika, ambayo ndio Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Endapo mtu ataikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na asiikubali Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah au asiitekeleze kwa njia sahihi hatokuwa muislamu wala mpwekeshaji. Bali atakuwa kafiri mkanushaji. Hayo ndio tutayazungumzia katika sura inayofuata – Allaah (Ta´ala) akitaka.

[1] 20:49-50

[2] 32:07

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 35-36
  • Imechapishwa: 06/02/2020