15. Sunnah na Bid´ah haviwi pamoja


6- Tambua ya kwamba watu kamwe hawakuzusha Bid´ah isipokuwa waliacha Sunnah kiasi chake. Tahadhari Muhdathaat, kwani hakika kila Muhdathah ni Bid´ah, kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu na watu wake ni Motoni.

MAELEZO

Hili ni kwa kuwa Sunnah na Bid´ah haviwezi kuwa pamoja isipokuwa kimoja kitatoa kingine. Mtu hawezi kuwa mzushi na wakati huo huo akawa Sunniy. Ima atakuwa mzushi au Sunniy. Ni vitu viwili visivyoweza kukutana. Ni lazima kimoja kiondoshe kingine. Haya ni katika madhara ya Bid´ah, kwamba haiwezi kukutana na Sunnah. Kwa ajili hiyo, dalili ya hilo ni kwamba, utaona watu wa Bid´ah wanazichukia Hadiyth Swahiyh na wanazichukia Sunnah. Adui wao mkubwa ni yule mwenye kusema “Hadiyth fulani inakataza hili au inaharamisha hili.” Huyu ndio adui wao mkubwa na baya zaidi wanalosikia. Hawataki kuzikia Hadiyth au Sunnah ambazo zinakwenda kinyume na yale waliyomo. Hii ni alama ya kwamba Sunnah na Bid´ah haviwezi kukutana.

Ama mtu wa Sunnah anafurahi pale anaposikia Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hufurahia hilo. Anaongezewa kheri juu ya kheri na elimu juu ya elimu. Mtu wa Sunnah hufurahia Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati mtu wa Bid´ah huzikimbia Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hili ni jambo liko wazi kwa wazushi. Wanazipiga vita Sunnah kwa kuwa zinapingana na yale waliyomo. Huu ni uzowefu umeonekana kwao.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Sharh-is-Sunnah, uk. 35
  • Imechapishwa: 05/11/2017