16. Mwenye kufanya, kujifunza, kufunza au kuridhia uchawi

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

07 – Uchawi. Kunaingia pia Swarf na ´Atwf. Atakayeufanya au akawa radhi nao anakufuru. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ

“Na [hao Malaika wawili] hawamfundishi yeyote mpaka wamueleze: “Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru [kwa kufanya uchawi]”.”[1]

MAELEZO

Kichenguzi cha saba miongoni mwa vichenguzi vya Uislamu ni uchawi. Maana ya uchawi kilugha ni ibara ya kitu kimechojificha na ikakosekana sababu yake.

Maana ya uchawi Kishari´ah ni ibara ya kuzingua, mafundo, dawa na mapulizo. Unaathiri kwenye mioyo na miili. Unamfanya mtu kuua hata kufa. Unatenganisha kati ya wanandoa wawili[2].

Uchawi umeitwa uchawi kwa sababu mchawi anaathiri kwa kujificha. Mchawi anafanya uzinguzi na vifundo ambavyo vinaathiri kwa uficho kwenye mioyo na miili. Uchawi unaweza kuathiri kwa maradhi, kwa kuua na kwa kutenganisha kati ya wanandoa.

Mchawi ambaye ana uhusiano na mashaytwaan ni lazima atumbukie ndani ya shirki. Ni aina moja wapo ya shirki. Kwa sababu mchawi ambaye ana mafungamano na mashaytwaan ni lazima baina yao wawe na kubadilishana huduma; ni lazima kuwepo mikataba. Jini anafunga mkataba na mchawi na hivyo mtu ambaye ni mchawi anakuwa ni mwenye kukufuru kutokana na yale yanayopelekea katika mkataba huu. Mtu huyu hujikurubisha kwake kwa kufanya mambo ya ushirikina ambayo anamtaka kufanya. Kwa mfano jini linaweza kumuomba amchinjie, auweke msahafu kwenye najisi, aukojolee au ajikurubishe kwake kwa kufanya mambo mengine ambayo ni ya shirki. Kwa hiyo pale ambapo mchawi huyo atafanya shirki ndipo jini atamuhudumia kwa kumtekelezea matakwa yake; akimwamrisha ampige mtu kofi atampiga, amuue mtu atamuua, amletee khabar fulani na mengineyo basi atafanya hivo.

Kwa hiyo uchawi ni shirki. Atakayefanya uchawi, kujifunza nao, kuufunza, kuufanya au akawa radhi nao basi amekufuru. Kwa sababu mwenye kuridhia ni kama mtendaji. Yule mwenye kuridhia shirki ni mshirikina. Dalili ni manneo ya Allaah (Ta´ala) kuhusu kisa cha Malaika wawili ambao waliteremshwa ardhini na kuwapa watu mtihani:

وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ

“Na [hao Malaika wawili] hawamfundishi yeyote mpaka wamueleze: “Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru [kwa kufanya uchawi]”.”

Mtu anapowaendea na kuwaomba wamfunze uchawi humnasihi na kumkataza kwa makemeo makali na huku humwambia:

إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ

“Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru [kwa kufanya uchawi].”

Aking´ang´ania ndipo wanamfunza.

Vilevile maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَانُ وَلَـٰكِنَّ الشَّيَاطِينَ كَفَرُوا يُعَلِّمُونَ النَّاسَ السِّحْرَ

“Sulaymaan hakukufuru lakini mashaytwaan ndio waliokufuru; wanafundisha watu uchawi.”[3]

Wamekufuru kwa kile kitendo chao cha kuwafunza watu uchawi. Uchawi ni kufuru na kuritadi. Yule mwenye kufanya uchawi na kuuridhia ni kafiri.

[1] 02:102

[2] Tazama “Fath-ul-Majiyd” (02/463) na “Adhwaa´-ul-Bayaan” (04/45)

[3] 02:102

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tabswiyr-ul-Anaam bisharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 42-43
  • Imechapishwa: 15/04/2023