15. Radd juu ya utata wa kwamba mwenye kutamka shahaadah hawezi kukufuru kwa hali yoyote ile

Tatu: Miongoni mwa shubuha zao ni kufikiria kwao kwamba kule kutamka tu “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” kunamwingiza mtu Peponi. Haijalishi kitu hata kama mtu atafanya mambo ya kufuru na ya shirki yenye kukufurisha na huku wameshikamana na uinje wa maandiko yanayosema ya kwamba mwenye kutamka shahaadah mbili basi Moto ni haramu kwake. Jibu juu ya utata huu ni kwamba Hadiyth zilizotajwa zinafasiriwa kuwa inahusiana na yule mwenye kusema “hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah” na akafa katika hali hiyo na wakati huohuo hakuitengua kwa shirki. Bali ameitamka kwa moyo msafi kabisa kutoka moyoni mwake na wakati huohuo akakufuru vile vyenye kuabudiwa badala ya Allaah na istoshe akafa juu ya hali hiyo. Kama ilivyo katika Hadiyth ya ´Utbaan:

“Hakika Allaah ameuharamisha Moto kwa yule mwenye kusema “hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah” huku akitafuta kwa kusema hivo uso wa Allaah.”[1]

Katika “as-Swahiyh” ya Muslim imekuja:

“Mwenye kusema “hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah” na akakufuru vile vyenye kuabudiwa badala ya Allaah, basi imeharamika mali na damu yake na hesabu yake iko kwa Allaah.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefungamanisha kuharamika kwa mali na damu kwa kupatikana mambo mawili:

La kwanza: Atamke “hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah”.

La pili: Akufuru vile vyenye kuabudiwa badala ya Allaah.

Hakutosheka kutamka kutokana na maana peke yake. Bali ni lazima mtu atamke hivo na atendee kazi.

Kusema “Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah” ni sababu ya kuingia Peponi, kuokoka kutokamana na Moto na ndio muqtadha ya hilo. Lakini sababu na muqtadha haviwezi kufanya kazi yake isipokuwa mpaka sharti yahakikike na vikwazo viondoke. al-Hasan [al-Baswriy] aliulizwa:

“Kuna watu wanaosema kwamba mwenye kusema “hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah” ataingia Peponi.” Akajibu: “[Ni kweli] mwenye kusema “hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah” ambapo akatekeleza haki na faradhi zake ataingia Peponi.”

Wahb bin Munabbih alisema kumwambia ambaye alikuwa ameuliza:

“Je, ´hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah` si ndio ufunguo wa Pepo?” Akajibu: “Ndio, lakini hakuna ufunguo wowote isipokuwa uko na meno. Ukija na ufunguo ulio na meno, utafunguliwa, vinginevyo hutofunguliwa.”

Ni vipi basi mtu atasema kwamba kule kutamka tu “hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah” kunamtosha mtu kuingia Peponi ijapokuwa yule mtamkaji atakuwa ni mwenye kuwaomba wafu na kuwaomba uokozi wakati wa majanga? Jengine isitoshe hakufuru vile vyenye kuabudiwa badala ya Allaah. Huku ni kupotoka katika batili.

[1] Muslim (01/456).

[2] Muslim (01/53).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Haqiyqat-it-Tawhiyd, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 27/03/2019