15. Njia mbili anazokhofiwa muislamu


Khofu kwa muislamu ni kwa njia mbili:

Ya kwanza: Kutoyajua mambo haya, kutotaka kujifunza nayo na kutopambanua kati ya haki na batili.

Ya pili: Kuzungumza kuhusu Allaah pasi na elimu. Wengi katika wale wanaojifanya wasomi leo wamethubutu kuyaingilia masuala makubwa katika mambo yanayohusiana na ´Aqiydah na wakawa wanayaongelea na kuyatolea fatwa na kuwahukumu watu ujinga na upotevu.

Kwa hivyo ni wajibu kwa muislamu afuate njia ya Ahl-ul-Haq. Lakini hata hivyo hili haliwezekani isipokuwa mpaka kwa kusoma na kuielewa dini ya Allaah.

Haitoshi kwa mtu akayahifadhi maandiko. Kwa kuwa wako baadhi ya watu ambao wanahifadhi “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy na ya Muslim na vilevile “as-Sunan”. Lakini hata hivyo hawafahamu maana zake na wala hawajui tafsiri zake. Bali wanafasiri kwa tafsiri zao wenyewe au wanachukua tafsiri zake kutoka kwa wapotevu katika Khawaarij au Murji-ah. Hii ndio khatari. Elimu sio kwa kuhifadhi peke yake. Elimu ni kwa kuhifadhi pamoja na kuelewa na kujua maana. Kuhifadhi hakupatikani isipokuwa kwa kusoma na kuchukua elimu kutoka kwa wanachuoni na kusoma kwao. Hii ndio elimu na uelewa wa sahihi. Kwa hiyo ni wajibu kwetu kuyawekea umuhimu mkubwa mambo haya ili tusije kutumbukia katika yale waliyotumbukiaemo mapote haya potevu ambayo wamekuwa hawana shughuli nyingine hivi sasa isipokuwa porojo, kuwatia watu upotevuni, kuwatia watu katika Bid´ah, kuwatia watu katika maasi pasi na ujuzi, elimu na uelewa. Hapana hila wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Allaah. Hili ni jambo muhimu ambapo tunawajibika kulipa umuhimu, kuzindukana nalo na tusiishie tu kusoma vitabu au kuhifadhi matini na maandiko pasi na kufahamu maana zake na kuelewa hukumu zake na maelezo yake kupitia kwa wanachuoni. Khawaarij hawakupotea isipokuwa kwa njia hii ya kuhifadhi bila ya kufahamu. Ndio maana Imaam Ibn-ul-Qayyim amesema kuhusu wao:

Wana maandiko ambayo wana upungufu katika kuyaelewa

kwa hiyo upungufu ukawaingilia katika ujuzi

Wana maandiko na wanahifadhi. Wanasoma Qur-aan usiku na mchana. Wanaswali usiku mzima na wanafunga. Lakini hata hivyo hawana uelewa wala mizani japo chembe kidogo ya mbegu ya hardali. Ndio maana wakatumbukia katika waliyotumbukiaemo. Uelewa ni kule kuyafahamu maandiko. Kwa hivyo ni lazima kwa mtu azijue dawa kwanza, kisha uzijue sababu zilizopelekea katika maradhi hayo halafu ndio utoe dawa stahiki. Dawa ikikutana na maradhi inakuwa ni yenye kunufaisha – kwa idhini ya Allaah. Dawa isipokutana na maradhi inadhuru. Kwa hiyo mwanachuoni yuko katika manzilah ya daktari na mgonjwa. Ni lazima yapatikane yote mawili; aijue dawa na sehemu ya kuweka hiyo dawa na ampe kila mmoja dawa stahiki. Mfano huu ni wa sawa iwapo utauzingatia. Lakini hili linahitajia uelewa na ujuzi.

Ndugu zetu hii leo wanajiona wao ni waelewa zaidi kuliko wanachuoni. Kwa ajili hii ndio maana wakatumbukia katika waliyotumbukia. Hapana hila wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Allaah. Huu ndio mwenendo wa Khawaarij. Khawaarij walifikia mpaka kuwakufurisha Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) na wakaona kuwa Maswahabah hawako katika haki na hawaelewi kitu. Walikuwa wanaona kuwa hawana wivu kwa Allaah. Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

Ujinga ni maradhi yenye kuangamiza

dawa yake ni mambo mawili yenye kuendana sambamba

andiko kutoka katika Qur-aan na katika Sunnah

Tabibu wa hayo ni mwanachuoni ar-Rabbaaniy

Khatati hii leo ni kubwa.

Tunamshukuru Allaah kuona vijana leo wana bidii katika dini na wana mwamko, kama wanavosema wenyewe[1]. Lakini iwapo mwamko na bidii hizi havitoelekezwa basi yatakuwa ni mambo yenye kudhuru. Kwa hiyo ni lazima kuvielekeza, kuvirekebisha na watu wawe na uelewa juu ya dini ya Allaah ili iwe ni mwamko kweli uliojengeka juu ya ujuzi, elimu na fahamu. Vinginevyo mwamko huu utawadhuru waislamu wasipozinduka na wakawaelekeza vijana na ndugu zao katika dini ya Allaah.

[1] Tazama taaliki ya Shaykh wetu juu ya istihali ya “mwamko wa kiislamu” katika kitabu “al-Ijaabaat-ul-Muhimmah fiyl-Mashaakil al-Mulimmah” (01/194).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 28-30
  • Imechapishwa: 08/05/2018