Miongoni mwa haki za wanandoa wakati wa kufunga ndoa ni pamoja na ndoa kutangazwa na kufanywa hadharani na isifanywe kwa siri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Tangazeni ndoa.”[1]

Katika hayo ni pamoja na kuonyesha furaha na kufurahikia ndoa isiyomtia mume kwenye matatizo wala madeni. Inatakiwa iwe kwa kiasi cha uwezo wa mume bila ya upetukaji mipaka wala ziada. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kumwambia ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf:

“Fanya harusi hata kama itakuwa kwa kondoo.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye alikuwa mbora na mcha-Mungu zaidi katika viumbe vya Allaah, alikuwa na harusi. Wakati alipomuoa Swafiyyah bint Huyyay alikuwa na uji na tende katika harusi yake. Hii ilikuwa ni harusi ya nani? Ni harusi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Sikumuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufanya harusi kwa wanawake wake kama alivyofanya kwa Zaynab.”[3]

Harusi ya Zaynab ilikuwa kubwa. Hakuna yeyote katika wanawake wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliekuwa na harusi kama hiyo. Unafikiria harusi hii ilikuwa vipi? Gharama yake ilikuwa kiasi gani? Unafikiria ilikuwa kubwa kiasi gani? Ni kiasi ngapi ilikuwa? Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Alichinja kondoo.”[4]

Kondoo mmoja kwenye harusi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ndoa kama ilivyosemwa inatakiwa kutangazwa. Wanawake na wasichana wanatakiwa kupiga dufu na nyimbo nzuri. ar-Rubayyi´ bint Mu´awwidh (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuja kwangu asubuhi baada ya mimi kuoa. Akakaa kwenye kitanda changu kama jinsi wewe ulivokaa na mimi. Wasichana wadogo wakapiga dufu na kuimba kuhusu mababu zao waliouawa katika Badr mpaka walipofikia kusema: “Katika sisi kuna Mtume anayejua yatayotendeka kesho.” Hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa amesema: “Usiseme hivo. Sema mliyokuwa mkisema mwanzo.”[5]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamkubalia nyimbo yake lakini akamkataza aliyoyasema.

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) anaeleza jinsi alivyomwandaa mwanamke (ambaye hapo mwanzoni alikuwa ni msichana yatima anayeishi naye) ambaye alikuwa anataka kuolewa na mwanaume katika Answaar. Hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Hamna burudani yoyote? Answaar wanapenda burudani.”[6]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Mtamtuma na msichana atayepiga dufu?” Nikasema: “Aimbe nini?” Akasema:

“Tumekujieni, tumekujieni.

Tusalimieni tukusalimieni… “[7]

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anamfundisha atavyosema. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema pia:

“Tofauti kati ya halali na haramu ni mlio wa dufu.”

[1] Ibn Hibbaan (9/4066), al-Haakim (2/2748), Ahmad na wengine. Mnyororo ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim. al-Haythamiy amesema: ”Wanaume wa Ahmad ni waaminifu.” (al-Majma´ (4/531)). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Aadaab-uz-Zafaaf”, uk. 105.

[2] al-Bukhaariy (5167) na Muslim (1427).

[3] al-Bukhaariy (5168) na Muslim (1428).

[4] Muslim (1428).

[5] al-Bukhaariy (4001).

[6] al-Bukhaariy (5162).

[7] at-Twabaraaniy katika ”al-Awsat” (3/3265) na al-Khallaal katika ”al-Amr bil-Ma´ruuf wan-Nahiy ´an-il-Munkar”, uk. 35. al-Haythamiy amesema: ”Kwenye mnyororo kuna Rawwaad bin al-Jarraah ambaye ni mwaminifu kwa mujibu wa Ahmad bin Hanbal, Ibn Ma´iyn na Ibn Hibbaan. Hata hivyo kuna udhaifu kwake.” (al-Majma´ (4/532)). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (1995) na ”Tahriym Aalaat-it-Twarb”, uk. 133.

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliym ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqq-uz-Zawjayn, uk. 22-24
  • Imechapishwa: 24/03/2017