15. Ndio maana daima tunaipa umuhimu na kipaumbele Tawhiyd

Ni wajibu kwa walinganizi wanaolingania katika dini ya Allaah walipe umuhimu jambo la Tawhiyd.

Miongoni mwa mambo yanayohuzunisha moyo ni kwamba kuna kundi la wajinga wanaohoji eti ni kwa nini kutiliwa mkazo mkubwa kama huu kwa Tawhiyd na kwamba ni kwa nini badala yake watu wasitilie umuhimu mambo ya waislamu na kwamba waislamu wanauliwa ulimwenguni kote. Wanahoji kwamba eti sisi tumetilia mkazo juu ya kuvunja makuba, kuvunja misikiti iliyojengwa juu ya makaburi na mfano wa mambo kama hayo. Mwenye kusema hivi amesahau au amejisahaulisha maneno ya kiongozi wa Tawhiyd ambaye ni Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema:

وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعْبُدَ الْأَصْنَامَ

“Uniepushe mimi na wanangu kuabudu masanamu.”[1]

Ikiwa Ibraahiym, ambaye ndiye kiongozi wa Tawhiyd ambaye Allaah alimfanya yeye peke yake kuwa Ummah, sivyo tu bali amesema (´Azza wa Jall) juu yake:

وَإِبْرَاهِيمَ الَّذِي وَفَّىٰ

“Ibraahiym aliyetimiza.”[2]

pia akamwamrisha Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumfuata katika Tawhiyd yake. Jengine ni kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) alimpa mtihani wa kumchinja mwana wake ambapo akatekeleza amri Yake,  aliyavunja masanamu kwa mkono wake mtukufu na akawafanyia ukali washirikina. Pamoja na matukio yote haya na mengineyo lakini akawa ni mwenye kukhofu kutumbukia ndani ya shirki ambayo ni kuyaabudia masanamu, jambo ambalo ndio shirki kubwa. Tusemeje sisi? Ibraahiym at-Taymiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Ni nani mwenye kujiaminisha na shirki baada ya Ibraahiym?”[3]

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema kuhusu Hadiyth ya Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh):

“Muusa alisema: “Ee Mola wangu! Nifunze kitu kitachonifanya kukukumbuka na kukuomba kwacho.” Akasema: “Ee Muusa! Sema: “Hapana mwabudiwa wa haki mwingine isipokuwa Allaah.”[4]

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema katika “Kitaab-ut-Tawhiyd” kuhusu Hadiyth hii:

“Faida tunayopata ni kwamba Mitume wanahitaji kuzindushwa juu ya fadhilah za “Laa ilaaha illa Allaah.”[5]

Kwa hiyo ni lazima kutilia mkazo jambo hili na kulipa umuhimu mkubwa. Likisalimika jambo hili yanayokuja baada yake ni mepesi na sahali zaidi. Kusalimika kwa jambo hili ndio kunategemea kusalimika kwa matendo mengine baada yake. Lakini msingi huu ukiharibika, basi hakuna manufaa yoyote, kutengemaa wala kukubaliwa.

[1] 14:35

[2] 37:53

[3] Ibn Jariyr katika ”Tafsiyr” yake (17/17).

[4] Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh” yake (14/102) (6218).

[5] Tazama ”al-Qawl-ul-Mufiyd ´alaa Kitaab-it-Tawhiyd”, uk. 78-87 ya Ibn ´Uthaymiyn.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Usuwl-ud-Da´wah as-Salafiyyah, uk. 44-46
  • Imechapishwa: 11/08/2020