1- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna yeyote anayenyenyekea kwa Allaah isipokuwa Allaah humnyanyua.”

2- Ni wajibu kwa mwenye busara kulazimiana na unyenyekevu na kujiepusha na kiburi. Lau kunyenyekea kusingekuwa na sifa yoyote nzuri zaidi ya kwamba kila ambavyo mtu anazidi kunyenyekea ndivyo anavyozidi kuwa juu, basi ingetosha kuwa ni wajibu kuwa mnyenyekevu.

3- Kuna sampuli mbili za unyenyekevu; wenye kusifiwa na wenye kusemwa vibaya. Unyenyekevu wenye kusifiwa ni kuacha kuwadharau waja wa Allaah. Unyenyekevu wenye kusemwa vibaya ni kunyenyekea kwa mtu anayemiliki kitu cha kidunia kwa kutaraji kile kitu alichonacho. Aliye na akili anatakiwa kuhakikisha kamwe asiwe na unyenyekevu wenye kusemwa vibaya na badala yake daima awe na unyenyekevu wenye kusifiwa.

4- ´Umar bin al-Khattwaab amesema:

“Ambaye ananyenyekea kwa ajili ya Allaah basi Allaah atamnyanyua na kumwambia: “Eshi maisha yako, Allaah akupe maisha!” Kidogo hichi chenyewe kinajiona kidogo, wengine wanamuona mkubwa. Pindi mja anapokuwa na kiburi na akapitiliza basi Allaah humbwaga chini na kumwambia: “Twezeka, Allaah akutweze!” Mkubwa huyu yeye mwenyewe anajiona ni mkubwa, wengine wamauona ni mdogo.”

5- Kunyenyekea kwa ajili ya Allaah kuko aina mbili:

Ya kwanza: Mja kunyenyekea kwa Allaah pindi anapofanya kitendo chema ili asijione.

Ya pili: Mja kujidharau mwenyewe wakati anapoyafikiria madhambi yake kwa kiasi cha kwamba haoni yeyote ulimwenguni aliye na matendo mema madogo na madhambi mengi kama yeye.

6- Bakr al-Muzaniy amesema:

“Ee mwanangu! Lau nisingekuwa hapa kwenye msimu basi ningelitaraji watu kusamehewa.”

7- Ni wajibu kwa mwenye busara kutokuwa na kiburi kutokana na sifa mbaya zinazopatikana ndani yake. Moja wapo hamdharau yeyote mpaka kwanza ajivune mwenyewe na anajiona kuwa yeye ni bora kuliko wengine. Nyingine anaudharau ulimwengu. Yule asiyewadharau watu hatokuwa vilevile na kiburi juu yao. Tatu mtu anavutana na Allaah (´Azza wa Jall) juu ya sifa Yake. Kiburi na ukuu ni katika sifa za Allaah (´Azza wa Jall). Anayepingana na Allaah kwazo atatupwa Motoni. Isipokuwa ikiwa kama Allaah atamsamehe.

8- Yahyaa bin Khaalid al-Barmakiy ameseama:

“Sharifu pindi anapofanya ´ibaadah, anakuwa na unyenyekevu. Mbaya pindi anapofanya ´ibaadah, anakuwa na kiburi.”

9- Kila mtu anaweza kuwa na unyenyekevu. Kwa unyenyekevu kunafikiwa usalama na maelewano. Unyenyekevu unaondosha chuki na vifundo. Matunda ya unyenyekevu ni mapenzi kama ambavyo matunda ya kukinai ni raha. Unyenyekevu wa sharifu unamzidishia usharifu wake kama ambavyo kiburi cha mtu mbaya kinamzidishia ubaya wake. Ni vipi asiwe na unyenyekevu ambaye ameumbwa kwa tone la manii na baadaye anakuwa mzoga mchafu na baina ya hivyo viwili amebeba uchafu?

10- Ibn ´Uyaynah amesema:

“Lau kungesemwa waondoshwe wabora wa mji huu basi wangeliondoshwa wasiojulikana.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 59-61
  • Imechapishwa: 12/11/2016