15. Mtoto anatakiwa kufunzwa Uislamu tangu akiwa mdogo

Umeniomba kuandika kwa ufupi mambo ya wajibu ya dini ambayo yanatamkwa na ndimi, yakaitakidiwa na mioyo na kutendewa kazi na viungo vya mwili na yale mambo yaliyopendekezwa ambayo yamefungamana na mambo ya wajibu… – Mtunzi anamzungumzisha mwalimu wake wa Qur-aan. Hapa kunabainishwa sababu ya utunzi wa kitabu hiki na utangulizi wake. Kitabu kinazungumzia madhehebu ya Imaam Maalik na utangulizi unabainisha ´Aqiydah sahihi. Hapa anataja sababu za utunzi wa kitabu ni kwamba mwalimu wake, wakati alipoona busara, akili na ujuzi wake wa madhehebu ya Imaam Maalik, ndipo akamuomba aandike madhehebu ya Imaam Maalik kwa ufupi. Lengo ilikuwa awafunze wanafunzi zake ili wakusanye kati ya kuhifadhi Qur-aan, ´Aqiydah na Fiqh. Namna hii ndivo walivokuwa wakifanya Salaf. Walikuwa wakiwafunza watoto tangu wakingali wadogo. Walikuwa wakiwafunza ´Aqiydah na Fiqh ili wakulie juu ya hilo. Mdogo anahifadhi vyema zaidi kuliko mkubwa. Mkubwa anasahau wakati mtoto elimu inashika zaidi akilini mwake. Ndio maana walikuwa wakisema kwamba elimu kipindi cha utoto ni kama kuchonga kwenye jiwe. Walikuwa wakipupia kuwafunza watoto ili elimu ikite na akulie juu yake. Namna hii waislamu ndivo wanavotakiwa kuwatilia umuhimu watoto wao na wawafunze ´Aqiydah na Fiqh. Haya ni tofauti na yale yanayosemwa na walezi wa kimagharibi kwamba watoto wasifunzwe chochote kinachohusu dini kwa sababu hawastahimili jambo hilo. Hizi ni njama ili watoto wa waislamu waleleke juu ya ujinga juu ya dini na ´Aqiydah yao na hukumu zinazohusu dini yao. Hili linapaswa kuzinduliwa. Hapo kitambo na si kale sana watoto wa waislamu walikuwa wakisoma na wakihifadhi vitabu vya ´Aqiydah katika shule za misingi. Vitabu hivi vilikuwa vikishereheshwa kwao. Mpaka kulipokuja walezi wa kisasa na mafunzo ya kimagharibi ndio yakashika mkondo. Wakageuza mifumo ya kimasomo katika nembo fulanifulani. Wako na misemo kama ´Aqiydah, Hadiyth na Fiqh, majina yasiyokuwa na maana yoyote. Hii ni ghushi katika kuwafunza watoto wa waislamu ili wapate kukua hali ya kuwa ni wajinga juu ya dini na ´Aqiydah yao.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 18-19
  • Imechapishwa: 07/07/2021