15. Msimamo juu ya Hadiyth zisizofahamika

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Yule menye kufikiwa na Hadiyth ambayo haielewi basi atambue kuwa kuna wenye kuielewa na kuitambua kwa ajili yake. Linalompasa ni kuiamini na kuisadikisha. Mfano wa Hadiyth hizo ni Hadiyth ya “mkweli na msadikishwaji”[1] na Hadiyth kuhusu Qadar na Hadiyth nyengine zote kuhusu Kuonekana. Haijalishi kitu hata kama kuna ambao hawawezi kuzisikia au kuchukulia kwa ubaya kuzisikiza. Lililo juu yake ni kuziamini na asirudishe herufi hata moja kwenye Hadiyth hizo au nyenginezo zilizopokelewa kutoka kwa wapokezi waaminifu.”

MAELEZO

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

“Allaah hakalifishi nafsi yoyote zaidi ya vile iwezavyo.”[2]

Kunaweza kuwepo baadhi ya maandiko ambayo huyaelewi. Ni yapi malengo yake? Ni ipi hekima yake? Lililo juu yako ni kuamini na kusadikisha. Hii ndio imani na kusadikisha inachohitajia. Wewe unaamini mambo yaliyofichikana na unaamini kuwa Muhammad ni haki na kwamba Qur-aan ni haki na ujumbe wa Muhammad ni wa haki na kwamba hazungumzi kutoka kichwani mwake. Yale unayoyajua, umeyajua, na yale usiyoyajua, yapeleke kwa mwanachuoni akufanyie nayo kazi.

[1] ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), naye ndiye mkweli na mwenye kusadikishwa, ametueleza: “Hakika umbo la kila mmoja wenu linakusanywa  pamoja katika tumbo la mama yake kwa muda wa siku arubaini. Kisha baadaye tone la damu kwa muda kama huo. Kisha tena huwa ni kipande cha nyama kwa muda kama huo. Halafu anatumiwa Malaika ambaye anaamrishwa kuandika mambo mane; rizki yake, maisha yake, matendo yake na kama atakuwa ni mwenye furaha au mla khasara.” (al-Bukhaariy (6549) na Muslim (2643))

[2] 02:286

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 377-378
  • Imechapishwa: 30/07/2017