15. Matendo na maneno ya mja yameumbwa na Allaah

Kuna watu wanaweza kutatizwa na kuuliza ni vipi matendo na maneno yetu yatakuwa ni ya khiyari ikiwa yameumbwa na Allaah (´Azza wa Jall). Mambo ni hivyo kwa kuwa matendo yetu na maneno yetu yanatokamana na mambo mawili:

1- Uwezo.

2- Kutaka.

Ikiwa kitendo cha mtu kinatokamana na utashi na uwezo wake, basi Allaah (´Azza wa Jall) ndiye ambaye ameumba utashi huu kwenye moyo wake. Allaah (´Azza wa Jall) pia ndiye ambaye ameumba uwezo ndani yake. Anaumba sababu kamilifu inayofanya kupatikana kwa matokeo. Ambaye kaumba sababu hii ndiye ambaye kaumba matokeo. Allaah (Ta´ala) kuumba kitendo cha mja ni kwa njia ya kwamba kitendo na neno la mja yanatokamana na mambo mawili:

1- Uwezo.

2- Kutaka.

Asingeliweza kufanya pasi na kutaka na pasi na uwezo. Anayetaka kutenda lakini akawa si muweza hatoweza kufanya kwa kuwa si muweza. Vilevile ambaye ni muweza lakini akawa si mwenye kutaka hatoweza kutenda. Kwa vile kitendo kimetokamana na utashi wa maazimio na uwezo mkamilifu, basi Allaah ndiye ambaye ameumba utashi wa maazimio na uwezo mkamilifu. Kwa njia hii tunapata kujua ni vipi Allaah (Ta´ala) anaumba matendo ya mja. Vinginevyo si mwingine ila mja ndiye mwenye kutenda; yeye ndiye mwenye kujisafisha, yeye ndiye mwenye kuswali, yeye ndiye mwenye kutoa zakaah, yeye ndiye mwenye kufunga, yeye ndiye mwenye kuh

iji, yeye ndiye mwenye kufanya ´Umrah, yeye ndiye mwenye kuasi na ndiye mwenye kutii. Lakini matendo yote haya yamepatikana kupitia matakwa na uwezo ambavyo vimeumba Allaah (´Azza wa Jall). Mambo yamekuwa wazi na himdi zote ni za Allaah.

Tunasema kuwa moto unaunguza, lakini Allaah (Ta´ala) ndiye kaumba kuunguza kwake. Hauunguzi peke yake. Unaunguza kwa kuwa Allaah (Ta´ala) ndiye kaufanya uunguze. Kwa ajili hiyo moto ambao Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitupwa ndani yake haukuwa wenye kuunguza. Kwa kuwa Allaah (Ta´ala) aliuambia:

قُلْنَا يَا نَارُ كُونِي بَرْدًا وَسَلَامًا عَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ

“Tukasema: “Ee moto! Kuwa baridi na salama juu ya Ibraahiym.””[1]

Hivyo ukawa ni baridi na salama kwa Ibraahiym. Kwa hiyo moto kivyake hauunguzi. Allaah (Ta´ala) ndiye kaumba ndani yake nguvu za kuunguza. Nguvu za kuunguza katika mkabala wa matendo ya mja ni sawa na matakwa na uwezo wao. Kupitia matakwa na uwezo ndio kunakuwa kitendo. Kupitia ala za kuunguza ndio kukawa kuunguza. Hakuna tofauti kati ya hali hizo mbili. Kwa vile mja ana utashi, hisia, khiyari ya kuchagua na kutenda, ndio kitendo kikawa ni chenye kunasibishwa kwake kihakika na kwa ajili hiyo akawa ni mwenye kuadhibiwa kwa yale anayoyafanya. Kwa kuwa anafanya na kuacha kwa khiyari.

[1] 21:69

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Qadhwaa’ wal-Qadar, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (5/225-226)
  • Imechapishwa: 25/10/2016