15. Maswali kuhusu kisa cha uongo cha kusulubiwa msalabani

Nimetaja baadhi ya ushabiki wa watu wenye dini wao kwa wao. Bado nina visa vingi vya kuelezea. Moja wapo inahusiana na mmoja katika ndugu vijana ambaye alikuwa akihudhuria katika darsa zangu. Anafanya kazi kama mhandisi huko Baghdaad. Nadhani kwamba anaitwa Tahsiyn. Baba yake alikuwa akiitwa ´Abdul-Qaadir, hilo nina yakini nalo. Ilikuwa mwaka wa 1955 au 1956.

Akanieleza kuwa baba yake alikuwa akifanya kazi katika idara ya serikali na kwamba kuna mkristo ambaye alikuwa akifanya nae kazi. Mkristo yule siku zote alikuwa akiutukana Uislamu ili kumchokoza ´Abdul-Qaadir. Siku miongoni mwa siku akasema:

“Sijawahi kuona watu walio wapunguani kama nyinyi waislamu. Mnadai kuwa Masihi hakuuawa na mayahudi. Mayahudi wameafikiana juu ya hilo. Sisi wakristo, pasi na kujali mielekeo yetu, tumeafikiana juu ya hilo. Wafuasi wa dini zote za ulimwenguni wameafikiana juu ya hilo kwa kuwa ni maelezo yaliyopokelewa kwa mapokezi tele. Nyinyi tu ndio wenye kukanusha hilo. Nyinyi ni kama ambaye anajaribu kuchonga ukuta kwa kichwa chake.”

Baba yake na Tahsiyn hakumjibu kitu. Akaenda nyumbani hali ya kuwa ni mwenye huzuni na ni mwenye kusikitika. Alipotengewa chakula cha jioni akakataa kula. Akawaeleza familia yake yaliyopitika. Kwa hiyo Tahsiyn akaniomba nimpe dalili kutoka kwenye Injili inayowakadhibisha wakristo na mayahudi na kuwathibitisha waislamu, kwa sababu wakristo wanadai kuwa wanaiamini Injili. Nikampa majibu yafuatayo:

Katika Matayo ya Injili mlango wa 26 na 27 inasema ya kwamba wanawazuoni wa mayahudi walimtuhumu ´Iysaa bin Maryam kuwa amekufuru na kwamba anastahiki kuuawa kwa mujibu wa Shari´ah ya Taurati. Simulizi zao juu ya kusulubiwa kwenye msalaba kunafahamisha namna madai yao yalivyo batili. Mambo hayo yanaweza kufupishwa katika maswali ambayo ni lazima kwa mkristo huyu anayeutukana Uislamu ayajibu:

1- Wale waliomkatama ´Iysaa, kama mnavyodai, walikuwa wanamjua ni nani au walikuwa hawamjui? Matayo ya Injili yanathibitisha kuwa walikuwa hawamjui.

2- Hayo yalipitika usiku au mchana? Matayo ya Injili yanathibitisha kuwa yalipitika usiku.

3- Ni nani ambaye kawaelekeza kwake? Matayo ya Injili yanathibitisha ya kwamba ilikuwa ni Yuda Iskariote, mmoja katika wale wanafunzi wake kumi na mbili.

4- Alifanya hivo bure au kwa pesa? Matayo ya Injili yanathibitisha ya kwamba alifanya hivo kwa pesa sawa na vipande thelathini vya fedha.

5- Ni vipi ilikuwa hali ya Masihi usiku huo? Matayo ya Injili yanasema hivi:

“Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka. 38Ndipo akawaambia: “Roho yangu ina huzuni mwingi kiasi cha kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.” 39Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli na kuomba: “Baba yangu, ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke. Lakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.”[1]

Haya hayawezi kusemwa na mtu ambaye anamuamini Allaah, sembuse Mtume wa Allaah. Waumini wanaitakidi kuwa Allaah juu ya kila kitu ni muweza.

6- Hali ya mwanafunzi wake wa kumi na mbili usiku huo huo ilikuwa vipi? Matayo ya Injili inasema:

“40Akarudi kwa wale wanafunzi na akawakuta wamelala, akamwambia Petro: “Hivi hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?”[2]

Hii ndio ilikuwa hali yao, kwa madai yenu, pamoja na kuwa ustadhi wao walikuwa katika mfazaiko.

7- Je, ´Iysaa (´alayhis-Salaam) alikuwa ni mwenye kuridhia hali zao? Hapana, Matayo ya Injili haisemi hivo:

“Roho yangu ina huzuni mwingi kiasi cha kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.” 39Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli na kuomba: “Baba yangu, ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke. Lakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. 41Kesheni, ombeni msije mkatiwa majaribioni. Roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.” 42Akaenda tena mara ya pili na akaomba kwa mara ya pili: “Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, basi yaache mapenzi yako yatimizwe.” 43Aliporudi tena akawakuta wamelala; kwa maana macho yao yamekuwa mazito. 44Akawaacha tena, akaenda na kuomba kwa mara ya tatu akisema maneno yale yale. 45Kisha akarudi tena kwa wanafunzi wake na kuwaambia: “Mmelala na kupumzika. Lakini saa imekaribia na Mwana wa Adamu ataachwa kwenye mikono ya wenye dhambi. 46Ondokeni, twende zetuni. Hapa anakuja yule atayenisaliti.”[3]

Sifa hizi haziendani na wanafunzi wema wa mwanachuoni na mtu mwema, sembuse wanafunzi wa Masihi (´alayhis-Salaam).

8- Je, walimsaidia pindi makutano walipomkamata? Kwa mujibu wa Matayo ya Injili walimkosesha nusura na kumkimbia:

“55Saa ile Yesu akawaambia makutano: “Mmetoka kama kumkamata mnyang’anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika? Siku zote niliketi hekaluni nikifundisha pasi na kunikamata. 56Lakini haya yote yamekuwa ili maandiko ya Manabii yatimizwe.” Ndipo wanafunzi wote wakamwacha na kumkimbia.”[4]

9- Je, ´Iysaa alikuwa na dhana nzuri juu ya wanafunzi wake usiku ule? Matayo ya Injili inasema:

“69Petro alikuwa ameketi nje behewani. Kijakazi mmoja akamwendea na kusema: “Wewe nawe ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.” 70Lakini akayakana mbele ya wote na kusema: “Sielei unachokisema.” 71Naye alipotoka nje mlangoni, kuna mwanamke mwingine alimuona, akawaambia watu waliokuwa huko: “Huyu alikuwa pamoja na Yesu Mnazareti.” 72Akakana tena kwa kiapo: “Simjui mtu huyu.” 73Punde kidogo wakamwendea wale waliohudhuria mpaka mbele ya Petro na kusema: “Hakika wewe pia ni mmoja wao. Kwa sababu yanasikika hata katika usemi wako.” 74Ndipo akaanza kulaani na kuapa akisema: “Simjui mtu huyu.” Na mara akawika jogoo. 75Ndipo Petro akalikumbuka lile neno la Yesu alilolisema: “Kabla ya kuwika jogoo utanikana mara tatu”, akatoka nje na kulia kwa majonzi.”[5]

10- Vipi makutano yalimkamata? Matayo ya Injili inasema:

“62Kisha akasimama kuhani mkuu na kumwambia: “Huna lolote la kujibu? Hawa wanakushuhudia nini?” 63Lakini Yesu akanyamaza. Kuhani mkuu akamwambia: “Nakuapisha kwa jina la Mungu aliye hai utwambie kama wewe ndiye Masihi, mwana wa Mungu.” 64Yesu akajibu: “Wewe ndiye umesema. Lakini nawaambieni: Baada ya haya mtamuona mwana wa Adamu amekaa upande wa mkono wa kuume wa Nguvu na akija juu ya mawingu ya mbinguni.” 65Ndipo kuhani mkuu akararua mavazi yake na kusema: “Amekufuru. Mna haja gani tena ya mashahidi?” Tazameni, sasa nyinyi wenyewe mmesikia hiyo kufuru yake. 66Mnaonaje?” Wakajibu: “Anastahiki kuuawa.” 67Ndipo wakamtemea mate usoni na wakampiga makonde na wengine wakampiga makofi 68wakisema: “Ewe Masihi, onyesha kama uko Nabii: ni nani aliyekupiga?”[6]

11- Ni nani aliyehukumu auawe? Matayo ya Injili inasema kuwa ilikuwa ni mgiriki na mrumi Pilato ambaye ndiye alikuwa akihukumu Palestina wakati huo:

“1Ilipokuwa asubuhi wakuu wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri juu ya kujaribu kumuua Yesu. 2Wakamfunga, wakamchukua na kumpeleka kwa Pilato, aliyekuwa liwali.”[7]

12- Wakati makutano walipokuja naye kwa Pilato na kumweleza ya kwamba wanawazuoni wa mayahudi wamemhukumu kumuua kwa kumsulubu kwa mujibu wa hukumu ya Taurati, je, aliwaamini kichwa kibubusa au alipeleleza hali ilivyo? Matayo ya Injili inasema:

“11Naye Yesu akasimama mbele ya liwali; liwali akamuuliza: “Wewe ndiye mfalme wa mayahudi?” Yesu akamjibu: “Wewe ndiye umesema hivo.” 12Pindi aliposhitakiwa na wakuu wa makuhani na wazee hakujibu kitu. 13Hapo ndipo Pilato akamwambia: “Husikii ni yepi wanayokushuhudia?” 14Hakujibu hata neno moja, hata liwali akastaajabu sana.”[8]

Hakusema kweli. Hata kama asingelikuwa Nabii wala Mtume ilikuwa ni wajibu kusema kweli na kujitakasa kutokamana na tuhuma za mayahudi:

“19Alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu mkewe alimpelekea mjumbe kumwambia: “Usiwe na lolote na yule mwenye haki, kwa sababu nimepata ndoto mbaya usiku kwa ajili yake.”[9]

Kwa mujibu wa Injili alikuwa akiwatolea mayahudi hotuba ndefu na akiwakaripia, akiwakemea na kuwatuhumu kwa ukali. Ni vipi leo ataacha kubainisha haki pindi liwali alipomuuliza ilihali anataka kuinusuru haki?

13- Kusulubiwa kulikuwa vipi? Matayo ya Injili inasema:

“38Wakati huo huo wanyang’anyi wawili wakasulibiwa pamoja naye, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wake wa kushoto. 39Waliokuwa wakipita njiani wakimtukana na wakitikisatikisa vichwa vyao 40wakisema: “Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu – jiokoe nafsi yako, kama kweli wewe ni mwana wa Mungu, shuka msalabani.”[10]

14- Swali hili ni balaa kubwa; alisema nini alipokuwa amesulubiwa msalabani? Matayo ya Injili inasema:

“45Karibu na saa sita palikuwa giza juu ya nchi yote mpaka saa tisa. 46Karibu na saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema: “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (Maana yake: Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha?).”[11][12]

Hii ni kufuru kwa mujibu wa wafuasi wa dini zote. Mwenye kusema ya kwamba ni Nabii ndiye alisema hivo ni kafiri kwa mujibu wa dini zote za kimbingu.

Tahsiyn akaenda na kumpa majibu baba yake na kumwambia:

“Mwalimu wetu Dr. al-Hilaaliy anakuomba umwambie: Ukiwa ni mkweli katika unayoyadai, basi yajibu haya maswali kwa njia nzuri na ya inswafu. Na kama unataka mdahalo, usijali nenda kwake.”

Baada ya Tahsiyn na baba yake kuyasoma maswali mara nyingi na kufurahishwa nayo, baba yake akamwendea yule mkristo na kumkadhibi yale maswali. Baada ya kuyasoma, akaonekana ni mwenye kujuta na akayaona makosa yake na akamuahidi ´Abdul-Qaadir kuwa kamwe hatorudi kuutukana Uislamu.

Haya ndio ninayoweza kukumbuka kutoka kwenye Matayo ya Injili niliyosoma tangu muda mrefu.

Himdi zote zinamstahiki Allaah. Swalah na salaam zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na wale wote wenye kuwafuata mpaka siku ya Qiyaamah.

[1] Matayo 26:37-39

[2] Matayo 26:40

[3] Matayo 26:38-46

[4] Matayo 26:55-56

[5] Matayo 26:69-75

[6] Matayo 26:62-68

[7] Matayo 01-02

[8] Matayo 27:11-14

[9] Matayo 27:19

[10] Matayo 27:38-40

[11] Matayo 27:46

[12] Matayo 27:45-46

  • Mhusika: ´Allaamah Muhammad Taqiyy-ud-Diyn al-Hilaaliy al-Maghribiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Baraahiyn al-Injiylyyah ´alaa anna ´Iysaa daakhil fiyl-´Ubuudiyyah wa la hadhdhwa lahu fiyl-Uluuhiyyah, uk. 38-42
  • Imechapishwa: 16/10/2016