Kuna mapote mengi yamepinda katika kufasiri Qadar ikiwa ni pamoja na yafuatayo:

2 – Jahmiyyah na Jabriyyah. Wamefasiri Qadar kuwa mja ametenzwa nguvu kufanya matendo ambayo hana khiyari nayo, uwezo wala utashi. Wamesema ni kama mfano wa bendera inapokuwa hewani na majani ya mti ambapo upepo unayapeperusha pasi na yenyewe kutaka wala kuwa na khiyari. Hivi ndivyo wanavyosema Jabriyyah katika Jahmiyyah na wengineo.

2 – Pote hili limeenda kinyume na wao. Nao ni Mu´tazilah. Wamefasiri Qadar kwamba mja ndiye ambaye anaumba matendo yake mwenyewe. Wanaona kuwa Allaah hana uhusiano wowote na matendo ya mja. Mja ndiye ambaye anafanya kitu kwa kutaka kwake na uwezo wake mwenyewe. Khiyari na uwezo wake hayana mafungamano yoyote na matakwa ya Allaah. Baadhi yao wamepetuka mipaka mpaka wakafikia kusema kwamba Allaah anayajua mambo tu baada ya kuwa yameshatokea. Hawa ndio Mu´tazilah waliopindukia. Jina lao jingine wanaoitwa Qadariyyah wakanushaji.

Pote la kwanza linaitwa Jabriyyah. Pote la pili linaitwa Qadariyyah wakanushaji.

Pote la kwanza linathibitisha Qadar na likavuka mipaka kwayo na wakampokonya mja kuwa na uwezo. Pote la pili ambao ni Mu´tazilah wao ni kinyume ambao wamevuka mipaka katika matakwa ya mja na katika kuthibitisha matakwa yake. Wamefanya hivo kiasi cha kwamba wakafikia kumpokonya Allaah matakwa na uwezo Wake. Mapote yote mawili yamepotea na wamekosea kosa kubwa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mujmal ´Aqiydat-is-Salaf as-Swaalih, uk. 14-15
  • Imechapishwa: 24/05/2022