Lengo la kumi na tano: Kuzihisi neema za Allaah

Miongoni mwa malengo makubwa ya hajj ni kwamba inamlea muislamu kuweza kuzihisi neema za Allaah zilizo juu yake, kumuwafikisha yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) kutekeleza utiifu na kumjaalia akawa muislamu, akamfanya akawa ni mwenye kuhiji, mwenye kuleta Talbiyah na akamjaalia akawa ni mwenye kumkumbuka na mwenye kumshukuru. Yote haya ni neema za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na fadhilah Zake juu ya mja Wake. Lau isingelikuwa ni neema ya Allaah juu yake juu ya hajj basi aisngelihiji. Lau isingelikuwa ni neema ya Allaah juu yake kwa kumjaalia ni miongoni mwa waswaliji basi asingeliswali. Lau isingelikuwa ni neema ya Allaah juu yake kumfungulia kifua chake juu ya dini hii basi asingelikuwa ni katika watu wake:

أَفَمَن شَرَحَ اللَّـهُ صَدْرَهُ لِلْإِسْلَامِ فَهُوَ عَلَىٰ نُورٍ مِّن رَّبِّهِ

“Je, yule ambaye Allaah amemkunjulia kifua chake kwa Uislamu naye yuko juu ya nuru kutoka kwa Mola wake?”[1]

Uongofu ni neema na fadhilah ya Allaah ambayo anampa yule amtakaye katika waja Wake – na Allaah ni Mwingi wa fadhilah.

Matendo ya hajj na nembo zake kuu zinamkumbusha mja juu ya jambo hili na zinamfanya kuweza kuhisi neema hii ya kiungu na zawadi ya kiuola. Hivyo anamshukuru Allaah kwa fadhilah Zake na anamshukuru Allaah vilevile kumjaalia kuwa ni mwenye kuhiji, mwenye kuleta Talbiyah, muislamu na kumuwafikisha juu ya kitendo hichi na kumwongoza kwacho. Tazama mtitiriko wa Aayah za hajj katika Suurah “al-Baqarah” maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

لَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَبْتَغُوا فَضْلًا مِّن رَّبِّكُمْ ۚ فَإِذَا أَفَضْتُم مِّنْ عَرَفَاتٍ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ عِندَ الْمَشْعَرِ الْحَرَامِ ۖ وَاذْكُرُوهُ كَمَا هَدَاكُمْ وَإِن كُنتُم مِّن قَبْلِهِ لَمِنَ الضَّالِّينَ

“Hapana dhambi kwenu kutafuta fadhilah toka kwa Mola wenu. Basi mtakapomiminika kutoka ‘Arafah, basi mtajeni Allaah katika al-Mash´ar al-Haraam na mdhukuruni Yeye kama alivyokuongozeni kwani hakika hapo kabla mlikuwa ni miongoni mwa waliopotea.”[2]

Bi maana mdhukuruni Allaah hali ya kuwa ni wenye kuhisi neema ya Allaah juu yenu kwa kuwaongoza na kukuokoeni (Subhaanahu wa Ta´ala) kutoka katika upotevu. Lau isingelikuwa ni neema ya Allaah juu yenu basi msingeliongoka. Lau isingelikuwa Allaah kukuokoeni kutoka katika upotevu basi mgelikuwa katika wapotevu. Amesema (Ta´ala):

لَن يَنَالَ اللَّـهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَـٰكِن يَنَالُهُ التَّقْوَىٰ مِنكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ سَخَّرَهَا لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ ۗوَبَشِّرِ الْمُحْسِنِينَ

“Haimfikii Allaah nyama zake wala damu yake, lakini kinachomfikia ni uchaji kutoka kwenu. Hivyo ndivyo tulivyokufanyieni wepesi kwenu ili mpate kumtukuza Allaah kwa yale aliyokuongozeni na wabashirie wafanyao wema.”[3]

Bi maana muadhimisheni na mtukuzeni. Kwa msemo mwingine kutokana na kule Yeye kukuongozeni. Hakika kweli anastahiki ukamilifu wa sifa, himdi na maadhimisho.

Miongoni mwa malengo ya hajj ambayo mtu anatakiwa kuyahudhurisha moyoni mwake ni kukumbuka neema ya Allaah juu yake kumuongoza katika hajj, swalah, swawm na dini nzima.

Haya ndio malengo muhimu na makubwa zaidi ya hajj. Ninamuomba Allaah (´Azza wa Jall) atuwafikishe sote katika elimu yenye manufaa, matendo mema, kuhakikisha malengo haya, atuzidishie ujuzi na maarifa katika dini na atuwafikishe katika yale ayapendayo na kuyaridhia…

Du´aa yetu ya mwisho ni: himdi zote ni za Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na salaam zimwendee mja na Mtume wake; Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake wote[4].

[1] 39:22

[2] 02:198

[3] 22:37

[4] Asili ya kijitabu hiki ni muhadhara nilioutoa katika msikiti wa al-Khayf huko Minaa baada ya swalah ya Maghrib siku ya Tarwiyah mwaka wa 1430. Umeandikwa kutoka katika kanda na ukatolewa. Nimefanya baadhi ya marekebisho kwa kuondosha na kuongeza baadhi ya vitu. Nilipendelea ubaki katika usulubu wake wa muhadhara kama ulivyokuwa.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Maqaaswid-ul-Hajj, uk. 75-78
  • Imechapishwa: 22/08/2018