15. Jitahidi utafute kwa njia iliokuwa nzuri

65- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Enyi watu! Hakuna yeyote atakayekufa isipokuwa mpaka akamilishe riziki yake na maisha yake. Hivyo basi mcheni Allaah na jitahidini kutafuta kwa njia nzuri. Yaliyoko kwa Allaah hayafikiwi kwa maasi.”[1]

66- Wanachuoni wetu wamesema kuwa mwanaadamu ni dhaifu na muhitajiaji; hawezi kitu na hajui kitu. Alipokuwa mdogo Allaah alimtazama kupitia kwa wazazi wake au wengine mpaka alipoweza kujimudu mwenyewe. Kisha baada ya hapo hali yake ikabadilika; wakati fulani yuko katika hali nzuri na wakati mwingine ni mwenye kuhitajia. Hali yake ni yenye kubadilika hata wakati wa haja. Lililo tukufu zaidi ni moyo wake autegemeze kwa Allaah katika kutafuta riziki na kumuabudu kikweli na kumtegemea kuwa Yeye ndiye mtoshelezaji. Akiamini hivyo na hali yake ikawa ya sawa basi riziki itamjia hali ya kuwa ni yenye kumkimbilia.

67- Tafsiri ya:

“Hivyo basi mcheni Allaah na jitahidini kutafuta kwa njia nzuri.”

ina maana ya kwamba afanye hivo kwa njia ya kuashiria na sio kwa njia iliyotajwa. Ikiwa kweli mtu ataomba basi na aelekee kwa mtu ambaye kunatarajiwa kupata msaada wake.

68- Hata hivyo lililo tukufu zaidi ni mtu kufanya kazi kama anaweza. Wakati riziki ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) ilipoisha alitoka na akamuona myahudi aliyekuwa na ndoo. Akamwambia: “Nikutolee ndoo ikiwa kama nitaweza kupata tende moja kwa kila ndoo nitakayoitoa?” Yule myahudi akasema: “Ndio, fanya hivo.” ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) akafanya hivo. Alipopata pato lake akatupa zile ndoo na akashika njia yake.

69- Kadhalika ikiwa mtu yuko na kazi na anakula kutokana na riziki hiyo. Mtume wa Allaah Daawuud alikuwa akila kutokana na pato la kazi yake, kama jinsi imevyothibiti katika al-Bukhaariy na wengine.

[1] al-Baghawiy(4113) na Ibn Abiyd-Dunyaa katika “al-Qanaa´ah” (57).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 49-51
  • Imechapishwa: 18/03/2017