10- Ni wajibu kwa mwanamke mwenye hedhi pale anapotwaharika kuosha mwili wake wote. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kumwambia Faatwimah bint Abiy Hubaysh:

“Wakati hedhi inapokuja acha swalah. Pindi hedhi yako inapoisha jisafishe na uswali.”[1]

Uwajibu wa chini kabisa katika kuoga ni kulowa mwili mzima ikiwa ni pamoja na mashina ya kichwa. Hata hivyo bora zaidi ni iwe kwa mujibu wa Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati Asmaa´ bint Shakl alipomuuliza namna gani mwanamke ataoga baada ya kutwaharika na hedhi:

“Mmoja wenu atachukua maji na mkunazi wake ajitwaharishe vizuri. Kisha ajimiminie maji kichwani mwake na akisugue kichwa msuguo wa nguvu mpaka afikilie mashina ya kichwa chake. Halafu atamwagia juu yake maji. Baada ya hapo atachukua kitambaa kilichotiwa miski ajitwaharishe nacho.” Asmaa´ akasema: “Atajitwaharisha nacho vipi?” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ametakasika Allaah!” ´Aaishah akamwambia: “Utapitisha mahali palipokuwa damu.”[2]

Sio wajibu kufumua nywele ikiwa hazikukazwa sana kiasi cha kwamba kunachelea juu yake maji yasifike kwenye mashina ya nywele. Muslim amepokea kupitia kwa Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba alimwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

Mimi ni mwanamke mwenye misuko. Je, nizifumue kwa ajili ya kuoga janaba?” Katika upokezi mwingine imekuja “kwa ajili ya kuoga hedhi na janaba? Akasema: “Hapana. Hakika yakutosha kumwagia kichwa chako mateko matatu ya maji kisha utajimiminia maji mwilini na hapo unakuwa umetwaharika.”[3]

Mwanamke akitwaharika hedhi yake katikati ya wakati wa swalah basi ni wajibu kwake kuharakisha kuoga ili aweze kuwahi kutekeleza swalah kwa wakati wake.

Na akiwa katika safari na hana maji au ana maji lakini anaogopa madhara endapo atayatumia au ana maradhi na maji yanaweza kumdhuru, basi badala yake atafanya Tayammum mpaka pale kizuizi kitapoondoka. Baada ya hapo ni wajibu kwake kuoga.

Kuna wanawake ambao wanatwaharika na hedhi katikati ya wakati wa swalah na wanachelewesha kuoga mpaka wakati wa swalah nyingine. Hoja yao ni kwamba hawawezi kujitwaharisha vizuri katika wakati huu. Hii sio hoja wala udhuru. Anaweza kuoga kwa wajibu wa chini kabisa na kuswali kwa wakati. Kisha pale atapopata wakati wa kutosha anaweza kujitwaharisha vizuri.

[1] al-Bukhaariy (306).

[2] Muslim (332).

[3] Muslim (330).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Dimaa’ at-Twabiy´iyyah lin-Nisaa’ http://www.ibnothaimeen.com/all/books/article
  • Imechapishwa: 30/10/2016