15. Dalili ya elimu kabla ya kuzungumza na kutenda

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mlango: Elimu kabla ya kauli na kitendo. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ

 “Basi elewa kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako.”[1]

Akawa ameanza kwa elimu kabla ya kauli na kitendo.”

MAELEZO

al-Bukhaariy – Ni imamu Muhammad bin Ismaa´iyl bin Ibraahiym al-Bukhaariy akijinasibisha kwa al-Bukhaaraa ambao ni mji ulioko mashariki. Ni imamu wa Ahl-ul-Hadiyth na jibali wa kuhifadhi (Rahimahu Allaah). Ndiye mtunzi wa “as-Swahiyh” ambacho ndicho kitabu sahihi zaidi baada ya Qur-aan.

Elimu kabla ya kauli na kitendo – Kwa sababu matendo hayafai ikiwa hayakujengeka juu ya elimu. Kuhusu matendo yaliyojengeka juu ya ujinga hayamnufaishi mwenye nayo. Bali yatakuwa ni janga na upotevu kwa mwenye nayo siku ya Qiyaamah. Kwa hiyo ni lazima mtu atangulize kujifunza elimu kabla ya kuanza kutenda.

Dalili – Bi maana dalili ya kichwa cha khabari hichi ni maneno Yake (Ta´ala):

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ

“Basi elewa kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako.”

Kwa sababu ameanza kwa elimu. Maneno Yake (Ta´ala):

وَاسْتَغْفِرْ

“… na omba msamaha.”

Haya ni matendo. Kwa hiyo Yeye (Subhaanah) ameanza kwa elimu kabla ya matendo. Kwa sababu matendo yakitokana na ujinga basi hayamfai kitu mwenye nayo. Kwa hiyo mtu anapaswa kuanza kujifunza kwanza kisha ndio atendee kazi yale aliyojifunza. Hii ndio kanuni.

[1] 47:19

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 37-38
  • Imechapishwa: 26/11/2020