1- Mwenye kula au kunywa kwa kusahau basi funga yake ni sahihi na wala halazimiki kulipa kwa mujibu wa maoni yenye nguvu zaidi ya wanachuoni. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtu akisahau ambapo akala na kunywa, basi aikamilishe funga yake. Kwani si vyenginevyo Allaah ndiye kamlisha na kumnywesha.”[1]

Pia kutokana na yale yanayofahamishwa na Hadiyth kwamba aliyesahau halazimiki kulipa. Haya ndio maoni ya sawa wanayoonelea jamhuri ya wanachuoni.

2- Mwenye kuoga, kusukutua au alikuwa akipandisha maji kwenye pua na maji yakaingia kooni mwake bila kukusudia swawm yake haiharibiki. Kadhalika yule ambaye nzi itaruka na kuingia kooni mwake, vumbi barabarani, unga wa ngano na mfano wa hivo haviharibu swawm yake kwa kutokuweza kujiepusha navyo. Jengine ni kwa sababu hakukusudia, hakutaka wala hakuchagua mwenyewe. Allaah (Ta´ala) amesema:

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

”Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”[2]

3- Inafaa kwa mfungaji kuoga. Hayo ni kutokana na yale yaliyothibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Alfajiri ilikuwa ikimkuta naye yuko na janaba kutoka kwa mkewe. Kisha anaoga na kufunga.”[3]

4- Inafaa kwa mwenye kufunga kujimwagia maji juu ya kichwa chake kwa ajili ya kutaka kupata baridi kidogo na kusukutua kinywa. Abu Daawuud amepokea kupitia Hadiyth ya mtu mmoja katika Maswahabah aliyesema:

“Nilimwona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) huko al-´Arj akijimwagia maji juu ya kichwa chake kutokana na kiu au joto kali ilihali amefunga.”[4]

5- Mwenye kula au kunywa hali ya kuwa na mashaka juu ya kuchomoza kwa alfajiri na hakubainikiwa na kupambazuka kwake, basi funga yake ni sahihi na si lazima kulipa siku hiyo. Amesema (Ta´ala):

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ

“Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe wa alfajiri kutokana na uzi mweusi.”[5]

Ama kuhusu aliyekula au kunywa hali ya kuwa na mashaka juu ya kuzama kwa jua na haikubainika kwake kwamba limezama kweli na wala hakuwa na dhana yenye nguvu kwamba limezama, itampasa kuilipa siku hiyo. Kwa sababu kimsingi ni kwamba mchana bado unaendelea.

6- Inajuzu kwa aliyefunga kumbusu mke wake na kumkumbatia muda wa kuwa hachelei kuamka kwa matamanio yake na akatokwa na kitu katika hayo. Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Aiashah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Alikuwa akibusu ilihali amefunga. Alikuwa ni mmiliki zaidi kwenu wa haja zake.”[6]

Katika “as-Swahiyh” kupitia kwa Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema:

“Ilikuwa inatokea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwabusu baadhi ya wakeze ilihali amefunga” kisha akacheka.”[7]

Katika “as-Swahiyh” ya Muslim kupitia Hadiyth ya Hafswah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akibusu ilihali amefunga.”[8]

Katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Alikuwa akimbusu ilihali amefunga.”[9]

Hadiyth hizi zinathibitisha kwamba inafaa kwa mfungaji kubusu na kukumbatia na kwamba funga yake ni sahihi midhali hachelei kwa kukumbatia kwake au kubusu kutokwa na kitu katika manii au madhiy kwa sababu ni yenye kumtoka kwa haraka. Akikhofia kutokwa na kitu basi italazimika kwake kuacha kukumbatia na kubusu. Kwani ´Aiashah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Alikuwa ni mmiliki zaidi kwenu wa haja zake.”

Jengine ni kwa sababu kunamlinda mfungaji kutoiharibu swawm yake. Kitu ambacho jambo la wajibu halitimii isipokuwa kwalo basi nalo litakuwa ni wajibu.

  • Ikitokea mfungaji akabusu au akakumbatia ambapo akatokwa na manii, basi funga yake imeharibika. Kadhalika iwapo atatazamatazama ambapo akatokwa na manii funga yake imeharibika. Vivyo hivyo iwapo atajichua sehemu za siri akatokwa na manii swawm yake imeharibika. Ni lazima kwake kulipa siku hiyo. Hata hivyo halazimiki kutoa kafara. Kafara imewekwa kwa ajili ya kufanya jimaa tu.
  • Ama akifikiria tu ambapo akatokwa na manii au akatokwa na manii kwa sababu ya kutazama mara moja tu bila kukusudia na pasi na kukariri, swawm yake haiharibiki. Kwa sababu hakufanya hivo kwa kutaka kwake.

7- Mzee mtumzima mwanaume na mwanamke na vivyo hivyo mgonjwa mwenye maradhi yasiyotarajiwa kupona watakula na kila mmoja wao atatakiwa kulisha masikini kwa kila siku iliyowapita. Hapa ni pale ambapo hawawezi kufunga kwa mujibu wa maoni ya wanachuoni wengi. Wamesema japokuwa Aayah yenye kusema:

وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ

”Kwa wale wanaoiweza lakini kwa tabu watoe fidia.”[10]

imefutwa, lakini hata hivyo hukumu ya kulisha bado ni yenye kuendelea kufanya kazi kwa mzee na kwa mgonjwa ambaye maradhi yake si yenye kutarajiwa kupona.

8- Imependekezwa kwa ndugu kuwafungia maiti wao. Inasihi kuwafungia. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kufa na anadaiwa swawm, basi amfungie walii wake.”

Akitaka atamtolea chakula kwa kila siku moja aliyokuwa anadaiwa. Kwa hivyo ndugu huyu wa maiti amekhiyarishwa baina ya kumfungia na kumtolea chakula.

[1] al-Bukhaariy (1933) na Muslim (1155).

[2] 02:286

[3] al-Bukhaariy (1926) na Muslim (1109).

[4] Abu Daawuud (2365).

[5] 02:187

[6] al-Bukhaariy (1927) na Muslim (1106).

[7] al-Bukhaariy (1928).

[8] Muslim (1107).

[9] al-Bukhaariy (1929).

[10] 02:184

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswaru fiy Ahkaam-is-Swiyaam, uk. 22-26
  • Imechapishwa: 23/05/2019