Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

La pili: Hakika Allaah haridhii kushirikishwa pamoja Naye yeyote katika ´ibaadah Yake; si Malaika aliyekaribu wala Mtume

aliyetumwa. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Na kwamba misikiti yote ni ya Allaah, hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.” (al-Jinn 72 : 18)

MAELEZO

Suala la pili miongoni mwa yale mambo ambayo ni wajibu kwetu kuyajua ni kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) haridhii kushirikishwa pamoja Naye katika ´ibaadah Yake na yeyote. Bali Yeye pekee ndiye mwenye kustahiki kuabudiwa. Dalili ya hilo ni ile aliyoitaja mtunzi (Rahimahu Allaah) katika maneno Yake (Ta´ala):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Na kwamba misikiti yote ni ya Allaah, hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.” (al-Jinn 72 : 18)

Allaah (Ta´ala) amekataza mtu kumuomba yeyote asiyekuwa Allaah. Allaah hakatazi kitu isipokuwa hakiridhii (Subhaanahu wa Ta´ala). Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِن تَكْفُرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنكُمْ ۖ وَلَا يَرْضَىٰ لِعِبَادِهِ الْكُفْرَ ۖ وَإِن تَشْكُرُوا يَرْضَهُ لَكُمْ

“Mkikufuru basi tambueni kwamba hakika Allaah ni mkwasi kwenu na wala haridhii kufuru kwa waja Wake – na mkishukuru huridhika nanyi.” (az-Zumar 39 : 07)

فَإِن تَرْضَوْا عَنْهُمْ فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يَرْضَىٰ عَنِ الْقَوْمِ الْفَاسِقِينَ

“Mkiwaridhia, basi hakika Allaah haridhii watu mafasiki.” (at-Tawbah 09 : 96)

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) haridhii shirki na kufuru. Bali amewatuma Mitume na akateremsha Vitabu ili kupiga vita kufuru na shirki na kuviteketeza. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَقَاتِلُوهُمْ حَتَّىٰ لَا تَكُونَ فِتْنَةٌ وَيَكُونَ الدِّينُ كُلُّهُ لِلَّـهِ

“Na pambaneni nao mpaka kusiweko fitina na dini yote iwe kwa ajili ya Allaah.” (al-Anfaal 08 : 39)

Ikiwa Allaah haridhii kufuru na shirki, basi lililo la wajibu kwa muumini na yeye ni kutoridhika navyo. Kwa sababu muumini anatakiwa kupenda na kuchukia kwa mujibu wa kupenda na kuchukia kwa Allaah.  Hivyo akasirike kwa yale yanayomkasirisha Allaah na aridhike na yale yanayomridhisha Allaah (´Azza wa Jall). Ikiwa Allaah haridhii kufuru na shirki, basi haijuzu kwa muumini kuyaridhia.

Shirki ni jambo kubwa na la khatari. Allaah (´Azza wa Jalla) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakaye.” (an-Nisaa´ 04 : 48)

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ

“Hakika yule mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah atamharamishia Pepo na makazi yake yatakuwa ni Motoni. Na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kunusuru.” (al-Maaidah 05 : 72)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kukutana na Allaah bila ya kumshirikisha na chochote, ataingia Peponi, na yule mwenye kukutana na Allaah ilihali ni mwenye kumshirikisha na chochote, ataingia Motoni.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 33-34
  • Imechapishwa: 18/05/2020