15. Ahl-us-Sunnah hawadhuriki na mababaisho ya wapinzani

Huenda kukaja kikwazo kingine kwamba pengine watu wengi wenye nia nzuri wakaitikia mkusanyiko huu baada ya wao kubainikiwa na Sunnah. Lakini tatizo linakuja kuwa watu wengi watabaki ni wenye kugawanyika katika misikiti hii mingi kwa mujibu wa madhehebu tofauti na Sunnah. Kwa hivyo mkusanyiko huu mmoja hauwezi kuhakikishwa.

Ni kweli kuwa hili linaweza kutokea. Lakini ni jambo la wazi kabisa ya kwamba jukumu haliko juu ya wale walioihuisha Sunnah hii na kuwaita watu kwayo, bali ni kwa wale walioendelea kwenda kinyume nayo. Kwa hiyo wakemewe wao na si mwengine.

Ama kuhusu kundi la kwanza mkusanyiko wao ndio uliowekwa katika Shari´ah kwa sababu umejengeka juu ya Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa akisifu Kundi Lililookoka:

“Ni Mkusanyiko.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Ni wale wenye kufuata yale niliyomo mimi hii leo na Maswahabah zangu.”[1]

Hivyo basi hawatodhurika na wale wenye kwenda kinyume nao imgawa watakuwa ni wengi kuliko wao. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakutoacha kuwepo kikundi katika Ummah wangu chenye kushinda juu ya haki. Hawatodhurika na wale wenye kuwakosesha nusura mpaka itapokuja amri ya Allaah na wao bado wako juu ya hayo.”[2]

Muumini hatakiwi kujihisi upweke kwa sababu ya uchahe wa watu wenye kupita katika njia ya haki, kama ambavyo vilevile hadhuriki kwa idadi kubwa ya wapinzani. Imaam ash-Shaatwibiy amesema:

“Huu ndio mwenendo wa Allaah kwa viumbe; Watu wa haki ni wachache ukilinganisha na watu wa batili, hayo ni kutokana na maneno Yake (Ta´ala):

وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ

 “Wengi wa watu hawatoamini japokuwa utalipupa.”[3]

وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ

“Lakini ni wachache sana miongoni mwa waja Wangu wenye kushukuru.”[4]

Vilevile Allaah ataitimiza ahadi aliyomuahidi Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), nayo ni kwamba utarudi[5] kuwa kitu kigeni. Ugeni utakuwepo mpaka pale watu wake watakapotokomea au wakawa wachache. Hapo ni pale ambapo mema yatakuwa maovu na maovu yatakuwa mema na Sunnah ikawa ni Bid´ah na Bid´ah ikawa ni Sunnah. Yatapopitika hayo Ahl-us-Sunnah watakabiliwa na matusi na mashambulizi[6], kama jinsi ilivyokuwa mwanzoni wakikabiliwa na Ahl-ul-Bid´ah kwa matarajio ya kwamba wazushi wakusanyike katika upotevu. Lakini Allaah hataki wakusanyike mpaka kisimame Qiyaamah. Mapote kamwe hayatokuwa na umoja juu ya wingi wao na kwa kuikhalifu kwao Sunnah. Bali kutaendelea daima kuwepo Ahl-us-Sunnah mpaka Qiyaamah kisimame. Pamoja na kuwa mapote mengi ya upotevu yanawachukia na kuwajengea uadui na bughudha ili wapate kukubaliana nao, bado ni wenye kuendelea kupambana ili wakubaliane nao, lakini bado ni wenye kuendelea kupambana, kuvutana na kuzuia mchana na usiku. Ndio maana Allaah anawaongezea ujira mwingi na kuwalipa thawabu kubwa.”[7]

Ninamuomba Allaah (Ta´ala) atuthibitishe juu ya Sunnah na atufishe katika hali hiyo. Haya ndio ya mwisho yaliyonisahilikia kukusanya katika haraka hii – na himdi zote ni za Allaah, Mola wa walimwengu.

[1] Nzuri kupitia zengine. Imepokelewa na at-Tirmidhiy kupitia kwa ´Amr na ameifanya kuwa ni nzuri. Kadhalika imepokelewa na at-Twabaraaniy kupitia kwa Anas. Imetajwa pamoja na upokezi wa kwanza, ambao ni Swahiyh katika “Silsilah al-Ahaadiyth as-Swahiyhah” (204).

[2] Swahiyh na imepokelewa kwa mapokezi tele na ipo katika marejeo yaliyotangulia. Tazama “Mukhtaswar Swahiyh Muslim” (1095) na “Swahiyh al-Jaami´ as-Swaghiyr” (6177).

[3] 12:103

[4] 34:13

[5] Bi maana Uislamu. Anaashiria maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Uislamu ulianza hali ya kuwa ni mgeni na utarudi kuwa mgeni kama ulivyoanza – Twubaa kwa wageni!”

Ameipokea Muslim na wengineo. Imetajwa katika “as-Swahiyhah” (1273).

[6] Kama alivyofanya mtunzi wa “al-Iswaabah” baada ya kuchanganya mambo wakati alipokuwa akibainisha maoni yake juu ya swalah ya ´Iyd jangwani. Wamesema:

“Bado wapo waislamu wenye kuzihifadhi swalah zao na maamrisho ya dini yao. Baadaye kukaja kijikundi hichi kidogo na kikaanza kuwakaripia na kuwafarikisha.”

Zingatia namna ambavyo wamefanya kulingania katika Sunnah ni jambo lenye kutenganisha mkusanyiko. Usirushie wengine mawe ikiwa nyumba yako wewe ni ya vio.

[7] al-I´tiswaam (1/12-13).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swalaat-ul-´Iydayn, uk. 45-48
  • Imechapishwa: 13/05/2020