149. Lengo la Allaah kuwatuma Mitume ni ili wamwabudu Yeye pekee

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah Ameutumia kila Ummah Mtume, kuanzia kwa Nuuh mpaka kwa Muhammad, ili kuwaamrisha kumuabudu Allaah Peke Yake na akiwakataza shirki. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume [awaamrishe watu wake] kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut.””[1]

Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Twaaghuut ni kila chenye kuabudiwa, kinachofuatwa au kutiiwa ambacho mja anapindukia mipaka yake.”

MAELEZO

Wanaojifanya kuwa ni Mitume ni wengi. Lakini Allaah huwafedhehi na kufichua jambo lao na pia anawabainishia aibu yao kwa watu. Yule mwenye kuwasadikisha ni kafiri kwa sababu ni mwenye kumkadhibisha Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maafikiano ya waislamu juu ya kwamba utume umekhitimishwa kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Maneno yake (Rahimahu Allaah):

”Allaah ameutumia kila Ummah Mtume.”

Allaah ameutumia kila Ummah Mtume ili asimamishe hoja dhidi yao ili wasije kusema kuwa hawakufikiwa na mbashirikiaji wala mwonyaji. Amesema (Ta´ala):

وَمَا كُنَّا مُعَذِّبِينَ حَتَّىٰ نَبْعَثَ رَسُولًا

”Hatukuwa Wenye kuadhibu mpaka tumtume Mtume.”[2]

Allaah ameutumia kila Ummah miongoni mwa nyumati zilizotangulia Mtume. Amesema (Ta´ala):

وَإِن مِّنْ أُمَّةٍ إِلَّا خَلَا فِيهَا نَذِيرٌ

”Hakuna ummah wowote isipokuwa amepita humo mwonyaji.”[3]

Lakini tunapaswa kujua ni ipi Da´wah ya Mitume? Da´wah ya Mitume, kuanzia wa mwanzo wao mpaka wa mwisho wao, ilikuwa ni kulingania katika Tawhiyd. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume [awaamrishe watu wake] kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut.””

Kila mwenye au chenye kuabudiwa badala ya Allaah ni Twaaghuut. Kama itavyokuja huko mbele katika aina mbalimbali za Twawaaghiyt na kwamba miongoni mwa sampuli zake ni yule mwenye kuabudiwa badala ya Allaah ilihali ni mwenye kuridhia jambo hilo, kama itavyokuja huko mbele. Maana ya maneno Yake:

وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“… na jiepusheni na Twaaghuut.”

Bi maana jiepusheni kuyaabudu masanamu na makaburi. Hizi ndio Twawaaghiyt. Hii ni dalili yenye kufahamisha kuwa Da´wah ya Mitume wote, kuanzia wa mwanzo wao mpaka wa mwisho wao, ni yenye kutilia mkazo juu ya Tawhiyd. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi niabuduni.”[4]

يُنَزِّلُ الْمَلَائِكَةَ بِالرُّوحِ مِنْ أَمْرِهِ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ أَنْ أَنذِرُوا أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاتَّقُونِ

“Anateremsha Malaika kwa Roho kwa amri Yake juu ya amtakaye miongoni mwa waja Wake kwamba: “Onyeni ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Mimi, hivyo basi nicheni.”[5]

Da´wah ya Mitume wote ilikuwa katika Tawhiyd, kumwabudu Allaah peke yake na kukataza kutokamana na shirki. Hii ndio Da´wah ya Mitume.

Kisha baada ya Tawhiyd kunakuja Shar´ah mbalimbali katika mambo ya halali na ya haramu. Upambanzui wa Shari´ah ni wenye kutofautiana kwa kutofautiana kwa nyumati na haja zake. Allaah anafuta katika Shari´ah hizo kile akitakacho. Kisha zote hizo zikafutwa kwa Shari´ah ya Uislamu katika mambo ya halali, ya haramu, ´ibaadah mbalimbali, maamrisho na makatazo. Kuhusu msingi ambao ni Tawhiyd hakuna tofauti ndani yake wala hakufutwi kitu. Hii ndio dini ya Mitume wote kuanzia wa mwanzo wao hadi wa mwisho wao. Amesema (Ta´ala):

لِكُلٍّ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةً وَمِنْهَاجًا

“Kwa kila Ummah katika nyinyi Tumeujaalia Shari’ah na mfumo wake.”[6]

Dini ya Tawhiyd ni kumwabudu Allaah kwa yale aliyoyawekea Shari´ah katika kila wakati kutegemea na hali yake. Shari´ah fulani ikifutwa watu wanakwenda kwa ile iliokuja kufuta. Mwenye kung´ang´ania na akabaki juu ya ile iliokuja kufuta basi anakuwa kafiri. Kwa sababu kutendea kazi iliofutwa haiwi ni dini baada ya kufutwa. Ilikuwa ni dini yenye kuzingatia kabla ya kufutwa. Ikishafutwa haizingatiwi tena ni dini na dini inakuwa ni ile iliokuja kufuta. Kwa ajili hiyo Shari´ah ya Uislamu ikafuta zile Shari´ah zengine zilizokuwa kabla yake. Yule mwenye kubaki katika uyahudi au ukristo baada ya kutumilizwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kafiri. Kwa sababu anatendea kazi dini iliofutwa na kuisha wakati wake.

[1] 16:36

[2] 17:15

[3] 35:24

[4] 21:25

[5] 16:02

[6] 05:48

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 291-294
  • Imechapishwa: 22/02/2021