148. Hukumu ya mwenye kudai utume baada ya Muhammad


Mtume wa mwanzo wao ni Nuuh. Kuhusu Mtume wa mwisho ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amesema (Ta´ala):

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ

“Hakuwa Muhammad baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii.”[1]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”… na mimi ni Nabii wa mwisho – hakuna Nabii mwingine baada yangu.”[2]

Nyujumbe za mbinguni zimeishilia kupitia yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Baada yake hakutotumilizwa Mtume mwingine hadi kisimame Qiyaamah. Lakini Shari´ah yake ni yenye kubaki hadi kisimame Qiyaamah na dini yake ni yenye kubaki mpaka kisimame Qiyaamah, kama tulivyotangulia kutaja. Mwenye kudai kuwa ni Mtume baada ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi huyo ni kafiri. Na mwenye kumsadikisha naye ni kafiri kwa sababu hakuna Mtume mwingine baada yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Wako viumbe wengi waliodai utume baada yake ambapo Allaah akawafedhehi kwa njia ya kudhihirisha uongo wao. Kutokana na tunavojua wa mwisho wao ni al-Qaadiyaaniy ambaye ni Ahmad al-Qaadiyaaniy wa India ambaye hapo mwanzoni alikuwa akidai elimu na kufanya ´ibaadah. Kisha baadaye akadai kuwa ni ´Iysaa mwana wa Maryam kisha akadai kuwa ni Mtume. Hii leo yuko na wafuasi kwa jina Qaadiyaaniyyah ambao waislamu wamewakufurisha, wakawakataa na kuwazingatia kuwa ni pote la kikafiri lenye kutoka nje ya Uislamu. Shukurani zote njema ni za Allaah kuona kwamba ni wenye kukataliwa na kufukuzwa kutoka katika nchi za waislamu. Wana uchangamfu. Lakini uchangamfu wao ni wenye kushindwa.

 Kwa kifupi ni kwamba hakuna Mtume mwingine baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yule mwenye kudai kuwa ni Mtume ni mwongo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Hakutosimama Qiyaamah mpaka wajitokeze Dajjaaluun waongo karibu thelathini. Wote watadai kuwa ni Mitume wa Allaah.”[3]

[1] 33:40

[2] Abu Daawuud (4252) na at-Tirmidhiy (2219).

[3] al-Bukhaariy (3609) na Muslim (2923).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 290-291
  • Imechapishwa: 22/02/2021