147. Mtume wa kwanza ni Nuuh na wa mwisho ni Muhammad

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Wa mwanzo wao alikuwa ni Nuuh (´alayhis-Salaam) na wa mwisho wao alikuwa ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Dalili juu ya kwamba wa mwanzo wao alikuwa ni Nuuh (´alayhis-Salaam) ni Kauli Yake (Ta´ala):

إِنَّا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ مِن بَعْدِهِ

”Hakika Tumekufunulia Wahy kama tulivyomfunulia Nuuh na Manabii baada yake.”[1]

MAELEZO

Dalili kwamba wa mwanzo wao ni Nuuh ni maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ

”Hakika Tumekufunulia Wahy… ”

Hapa anazungumzishwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ مِن بَعْدِهِ ۚ وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالْأَسْبَاطِ وَعِيسَىٰ وَأَيُّوبَ وَيُونُسَ وَهَارُونَ وَسُلَيْمَانَ ۚ وَآتَيْنَا دَاوُودَ زَبُورًا

”… kama tulivyomfunulia Nuuh na Manabii baada yake na tumemfunulia Wahy Ibraahiym na Ismaa’iyl na Ishaaq na Ya’quub na kizzi, na ‘Iysaa na Ayyuub na Yuunus na Haaruun na Sulaymaan. Na Tumempa Daawuud Zabuur.”[2]

Allaah katika Aayah hii ametaja jumla katika majina yao kama alivyotaja jumla ya majina yao katika Aayah ya an-An´aam:

وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ ۚ كُلًّا هَدَيْنَا ۚ وَنُوحًا هَدَيْنَا مِن قَبْلُ ۖ وَمِن ذُرِّيَّتِهِ دَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ وَأَيُّوبَ وَيُوسُفَ وَمُوسَىٰ وَهَارُونَ

”Tukamtunukia Ishaaq na Ya’quub, wote tumewaongoza, na Nuuh tulimwongoza hapo kabla, na katika kizazi chake Daawuud na Sulaymaan na Ayyuub na Yuusuf na Muusa na Haaruun.”[3]

Wa mwanzo wao ni Nuuh (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Dalili ya hilo ni maneno Yake:

وَالنَّبِيِّينَ مِن بَعْدِهِ

”… na Manabii baada yake.”

Allaah alimtuma kwa watu wake pindi walipochupa mipaka kwa waja wema baada ya kwamba watu walikuwa katika dini ya Tawhiyd tokea kipindi cha Aadam (´alayhis-Salaam) kwa karne kumi wakiwa juu ya Tawhiyd. Walipokuja watu wa Nuuh ndani yake kulikuweko waja wema. Walipofariki waja wema hawa walihuzunika huzuni kubwa. Hapo ndipo shaytwaan alitumia fursa hiyo na akawaambia watengeneze picha za waja wao wema na wazitundike katika vikao vyao kwa lengo kwamba mkiona picha hizo mtazikumbuka hali zao na mtapata uchangamfu wa kufanya ´ibaadah. Wakasimama na kutengeneza picha za wafu hawa na wakazitundika kwenye vikao vyao. Mara ya mwanzo hawakuwaabudu kwa sababu walikuweko wasomi ambao walikuwa wakiwabainishia watu Tawhiyd na wakiwakemea shirki. Pindi walipokufa wasomi wale na kikaenda kizazi cha kwanza baadaye kulikuja kizazi wakati ambapo wale wasomi walikuwa wameshakufa. Shaytwaan alikuja na akawanong´oneza kwamba baba zao hawakutundika picha hizo isipokuwa kwa lengo waziabudu  na kwamba walikuwa wakiomba mvua kupitia picha hizo. Akawapambia kuziabudu na hivyo wakaziabudu badala ya Allaah. Matokeo yake ndipo kukatokea shirki ulimwenguni. Hapo ndipo Allaah alimtumiliza Mtume Wake Nuuh (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Waliambizana wasimtii Nuuh na matokeo yake wakaendelea juu ya ukafiri wao, ujeuri na ukaidi wao. Hiyo ndio ilikuwa shirki ya kwanza kuzuka ulimwenguni. Sababu yake ilikuwa picha. Kwa ajili hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakika watu wataokuwa na adhabu kali siku ya Qiyaamah ni watengeneza picha.”[4]

”Hakika wale Wanaotengeneza picha hizi wataadhibiwa siku ya Qiyaamah wataambiwa: ”Vipeni uhai mlivyoviumba.”[5]

Wataamrishwa kuzipulizia roho picha hizi kwa lengo la kuwafanya washindwe na kuwaadhibu. Kwa sababu picha ni njia miongoni mwa njia zinazopelekea katika shirki, kama ilivyowapitikia watu wa Nuuh.

[1] 04:163

[2] [2]

[3] 06:84-86

[4] al-Bukhaariy (5950) na Muslim (2109).

[5] al-Bukhaariy (5951) na Muslim (2108).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 287-290
  • Imechapishwa: 18/02/2021