146. Hukumu ya wanaomkubali Mtume lakini wakadai kwamba ametumwa kwa waarabu pekee

Atakayedai kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametumwa kwa waarabu peke yao – kama wanavyosema kundi katika manaswara – amemkufuru Allaah (´Azza wa Jall). Miongoni mwa manaswara wako wanaokubali kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Mtume kutoka kwa Allaah, lakini hata hivyo ujumbe wake ni kwa waarabu pekee, huyu ni kafiri kamkufuru Allaah (´Azza wa Jall). Kwa sababu amekanusha ueneaji wa ujumbe. Kwa ajili hiyo yule mwenye kudai utume baada ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kafiri. Kwa sababu Allaah (Jalla wa ´Alaa) amemfanya Muhamamd kuwa Mtume wa mwisho:

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ

”Hakuwa Muhammad baba wa mmoja yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii.” (al-Ahzaab 40)

Mwisho wa Manabii ni yule ambaye baada yake hakuji mwingine yeyote. Kwa ajili hii amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mimi ndiye Nabii wa mwisho, hakuna Nabii baada yangu. Baada yangu watakuwepo waongo thelathini na kila mmoja wao atadai kuwa ndio Nabii ilihali mimi ndiye Nabii wa mwisho. Hakuna Nabii baada yangu.”[1]

Watu hawana haja ya Nabii. Nabii hutumwa wakati watu wana haja naye. Kwa sababu Allaah kawatosheleza kwa Qur-aan na Sunnah itayoendelea mpaka kitaposimama Qiyaamah. Hivyo hawana haja ya Nabii na wala hawana haja ya Shari´ah kinyume na Shari´ah ya Muhamma (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Zama zimejaa Shari´ah ya Uislamu mpaka pale kitaposimama Qiyaamah. Ama Shari´ah za Manabii wengine zinatumiwa katika nyakati zake. Kila Shari´ah inahukumiwa katika wakati wake na haivuki wakati wake. Wakati wa Shari´ah hii ni mpana kuanzia alipotumilizwa mpaka Qiyaamah kitaposimama. Ni yenye kujitosheleza na ni yenye kufanya upya katika hukumu zake, Qur-aan na Sunnah zake. Watu hawana haja ya Mtume baada ya kutumwa kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), hawana haja ya Kitabu baada ya Qur-aan na wala hawana haja ya Shari´ah baada ya Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa ajili hiyo yule atakayedai kuwa ni Nabii au akamsadikisha mwenye kusema hivyo anakuwa kafiri mwenye kuritadi kutoka katika dini ya Uislamu. Anakuwa kamkadhibisha Allaah, Mtume Wake na maafikiano ya waislamu ambao wamekubaliana kwamba ujumbe ambao katumilizwa nao Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kwa watu wote. Kwa hivyo hakuna yeyote awaye awezaye kutoka katika Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] Ameipokea Ahmad (05/278)), at-Tirmidhiy (2219), Abu Daawuud (3252), Ibn Maajah (3952), al-Haakim (03/449) ambaye ameisahihisha juu ya masharti ya al-Bukhaariy na Muslim. at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 185-187
  • Imechapishwa: 12/03/2019