146. Dalili kwamba Allaah amewatumiliza Mitume wakiwa ni wenye kutoa bishara njema na kuonya


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah ametuma Mitume wote wakiwa ni wenye kutoa bishara njema na kuonya. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

رُّسُلًا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّـهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ عَزِيزًا حَكِيمًا

“Mitume wenye kutoa bishara njema na waonyaji ili pasikuweko kutoka kwa watu hoja yoyote juu ya Allaah baada ya kuletwa ya Mitume. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu kabisa, Mwenye hekima.”[1]

MAELEZO

Imani ya kuwaamini Mitume ni moja katika nguzo za imani sita. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Imani ni kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake na Mitume Yake.”

Kuwaamini Mitume ni moja katika nguzo sita za imani. Kwa hiyo ni lazima kuwaamini Mitume wote kuanzia wa mwanzo wao hadi wa mwisho wao. Yule mwenye kumpinga Mtume mmoja katika wao basi amewakufuru wote. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الَّذِينَ يَكْفُرُونَ بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَيُرِيدُونَ أَن يُفَرِّقُوا بَيْنَ اللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَيَقُولُونَ نُؤْمِنُ بِبَعْضٍ وَنَكْفُرُ بِبَعْضٍ وَيُرِيدُونَ أَن يَتَّخِذُوا بَيْنَ ذَٰلِكَ سَبِيلًا أُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ حَقًّا ۚ وَأَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا مُّهِينًا

“Hakika wale waliomkanusha Allaah na Mtume Wake na wanataka kufarikisha baina ya Allaah na Mtume Wake na wanasema: “Tunaamini baadhi na tunawakanusha baadhi”; na wanataka kuchukua njia iliyo baina ya hayo – hao ndio makafiri wa kweli. Na Tumewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha.””[2]

Kwa hiyo ni lazima kuwaamini Mitume wote kuanzia wa mwanzo wao hadi wa mwisho wao, kuamini wale ambao wametajwa na Allaah kwa majina ndani ya Kitabu Chake na wale ambao hawakutajwa kwa majina. Hakika Mitume ni wengi. Kwa ajili hii imepokelewa katika Hadiyth:

”Idadi yao ni laki moja na elfu ishirini na nne na Mitume ni mia tatu na kumi na tano.”[3]

Ni Mitume wengi. Miongoni mwao wako ambao Allaah amewataja kwa majina yao na wengine hakuwataja kwa majina yao. Ni lazima kuwaamini wote kuanzia wa mwanzo wao mpaka wa mwisho wao.

[1] 04:165

[2] 04:150-151

[3] Ahmad katika ”al-Musnad” (36/217-619) (22287).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 286-287
  • Imechapishwa: 18/02/2021