145. Shari´ah ya Muhammad ni yenye kutumika katika zama na mahali

Jengine ni kwamba tunatakiwa kutambua kwamba mambo ya kiada na mambo yaliyoruhusiwa hayaingii katika Bid´ah. Ni kama mfano wa mambo ya viwanda. Katika Qur-aan na Sunnah kumekuja yanayohusiana nayo. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَسَخَّرَ لَكُم مَّا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا مِّنْهُ

”Amekutiishieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini vyote humo.” (al-Jaathiyah 45:13)

Hata mambo yaliyoruhusiwa, mambo ya uvumbuzi, mambo ya maendeleo katika mambo ya viwanda na uvumbuzi yanajumuishwa na Qur-aan na Sunnah. Allaah ameashiria mambo ya kidunia katika Qur-aan na akasema watu wanufaike navyo na wavitumie. Lakini ufahamu na kuelewa kwa watu kunaweza kuwa na mapungufu juu ya haya. Kasoro inarudi katika ufahamu wa watu. Qur-aan na Sunnah vimekamilika, ni vyenye kuenea, vyenye kusilihi katika kila zama na mahali. Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni yenye kuenea na kamilifu. Jengine ni kwamba ni kwa watu na majini wote,  hakuna yeyote baada ya kutumwa kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoka katika Shari´ah yake. Pasi na kujali ni nani. Akitoka basi huyo ni kafiri.

“Hatosikia yeyote kuhusu mimi, si myahudi wala mnaswara, kisha asiamini yale niliyokuja nayo isipokuwa ataingia Motoni.”

Ikiwa haya ni kuhusu Ahl-ul-Kitaab, tusemeje kwa wengine? Kwa sababu vitabu vilivyotangulia vimekwisha na vimeshafutwa kwa Kitabu hichi Qur-aan tukufu. Hichi kimefuta vitabu vingine vyote. Shari´ah yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) imefuta Shari´ah zengine zote. Shari´ah zao zilikuwa za muda. Allaah (Jalla wa ´Alaa) huwawekea Shari´ah kila Ummah yale yanayoendana nao. Amesema (Ta´ala):

لِكُلٍّ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةً وَمِنْهَاجًا

“Kwa kila katika nyinyi Tumeweka Shari’ah na mfumo.” (al-Maaidah 05:48)

Kila watu Anawawekea Shari´ah inayoendana nao katika wakati wao. Kisha baadaye Shari´ah hiyo inaisha kwa kuja nyingine mpaka ilipokuja Shari´ah ya Uislamu. Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kuanzia wakati alipotumwa mpaka Qiyaamah kitaposimama. Ni yenye kuenea katika kila zama, ni yenye kuenea katika kila mahali na ni yenye kufanya kazi kwa waja mpaka pale kitaposimama Qiyaamah; haitobadilishwa na wala haitogeuzwa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 184-185
  • Imechapishwa: 12/03/2019