145. Kukusanyika nyumbani kwa maiti kwa ajili ya kula, kunywa na kusoma Qur-aan

Swali 145: Katika baadhi ya miji anapofariki maiti basi wanakusanyika nyumbani kwa maiti kwa muda wa siku tatu wakiswali na wakimwombea du´aa. Ni ipi hukumu ya hili[1]?

Jibu: Kukusanyika nyumbani kwa maiti kwa ajili ya kula, kunywa na kusoma Qur-aan ni Bid´ah. Vilevile kuswali nyumbani haijuzu. Bali ni lazima kwa wanamme kuswali msikitini pamoja na wengine. Wafiwa wa maiti wanaendewa kupewa mkono wa pole, kuombewa du´aa na kumwombea rehema maiti wao. Lakini kukusanyika kwa ajili ya matanga kwa ajili ya kufanya kisomo maalum, kuomba du´aa maalum na mengineyo ni Bid´ah. Lau mambo hayo yangelikuwa ni kheri basi wangetutangulia kwayo wema waliotangulia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakufanya hivo. Ja´far bin Abiy Twaalib, ´Abdullaah bin Rawaah na Zayd bin Haarithah (Radhiya Allaahu ´anhum) katika vita vya Mu´tah na akajiwa na khabari (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitia njia ya Wahy ambapo akawatangazia Maswahabah na akawaeleza juu ya kufariki kwao na akawaridhia na kuwaombea du´aa. Lakini hakuwafanyia matanga. Vivyo hivyo Maswahabah baada yake hawakufanya chochote katika hayo. Alifariki as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) na hawakumfanyia matanga. ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alifariki na hawakumfanyia matanga. Wala hawakukusanya watu wamsomee Qur-aan. Baada ya hapo akauliwa ´Uthmaan na ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) na Maswahabah hawakufanya chochote katika hayo. Sunnah ni kuwatengenezea chakula wafiwa wa maiti kutoka kwa jamaa au majirani zao kisha wawatumie. Kama alivofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipofikiwa na khabari za kufa kwa Ja´far akasema kuwaambia familia yake:

“Watengenezeeni familia ya Ja´far chakula. Kwani hakika wamefikwa na kitu kinachowashughulisha.”[2]

Wameipokea watano isipokuwa an-Nasaa´iy.

Haya ndio yamewekwa katika Shari´ah.

Kuhusu wao kubeba mabalaa juu ya mabalaa ambayo tayari wako nayo na kuwatia uzito wa kuwapikia chakula watu ni jambo linalokwenda kinyume na Sunnah. Isitoshe ni Bid´ah kutokana na yale tuliyoyataja.

Jariyr bin ´Abdillaah al-Bajaliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Tulikuwa tukizingatia kukusanyika nyumbani kwa maiti na kutengeneza chakula baada ya kuzika ni katika kuomboleza.”[3]

Ameipokea Imaam Ahmad kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

Kuomboleza (النياحة) ni kunyanyua sauti kwa kulia, jambo ambalo ni haramu. Maiti anaadhibiwa ndani ya kaburi lake kwa kufanyiwa maombolezi. Hivo ndivo imesihi Sunnah kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hivyo ni lazima kutahadhari kutokamana na hilo.

Kuhusu kulia hapana neno ikiwa ni kutiririkwa na machozi peke yake pasi na kuomboleza. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipofariki mwanawe Ibraahiym:

“Hakika macho hutokwa na machozi na moyo huingiwa na huzuni na wala hatusemi isipokuwa yale yenye kumridhisha Mola wetu. Hakika sisi ni wenye kuhuzunika kwa kutengana na wewe Ibraahiym.”[4]

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (13/383-385).

[2] Ahmad (1754), Ibn Maajah (1610), at-Tirmidhiy (998) na Abu Daawuud (3132).

[3] Ahmad (6866) na Ibn Maajah (1612).

[4] al-Bukhaariy (1303) na tamko ni lake, na Muslim (2315).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz, uk. 104-106
  • Imechapishwa: 23/01/2022