144. Baada ya watu kufufuliwa watahesabiwa na watalipwa kwa matendo yao

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Baada ya kufufuliwa watahesabiwa na watalipwa kwa matendo yao. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَلِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ أَسَاءُوا بِمَا عَمِلُوا وَيَجْزِيَ الَّذِينَ أَحْسَنُوا بِالْحُسْنَى

“Na ni vya Allaah Pekee vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini ili awalipe wale waliofanya uovu kwa yale waliyoyatenda na awalipe wale waliofanya wema kwa [kuwaingiza] Peponi.”[1]

MAELEZO

Miongoni mwa matendo ya siku ya Qiyaamah ni hesabu na mizani. Hesabu maana yake ni kuwahoji watenda maasi. Waislamu wamegawanyika mafungu yafuatayo siku ya Qiyaamah:

La kwanza: Wako ambao hawatofanyiwa hesabu na wataingia Peponi pasi na hesabu wala adhabu. Hivo ndivo ilivyopokelewa katika Hadiyth ya watu 70.000 ambao wataingia Peponi bila ya hesabu wala adhabu[2].

La pili: Wako ambao watafanyiwa hesabu nyepesi. Ni kule kuonyeshwa peke yake. Hawatofanyiwa hesabu ya kuhojiwa bali watafanyiwa hesabu ya kuonyeshwa peke yake. Hawa pia ni miongoni mwa wataopata furaha. Amesema (Ta´ala):

فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَسَوْفَ يُحَاسَبُ حِسَابًا يَسِيرًا وَيَنقَلِبُ إِلَىٰ أَهْلِهِ مَسْرُورًا

”Basi ama yule atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atahesabiwa hesabu nyepesi, na atageuka kwa ahli zake akiwa ni mwenye kufurahi.”[3]

La tatu: Wako ambao watafanyiwa hesabu ya mahojiano. Watu kama hawa watakuwa katika khatari. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Atakayohojiwa hesabu ataadhibiwa.”[4]

Kuhusu makafiri wanachuoni wametofautiana kama watafanyiwa au hawatofanyiwa hesabu. Miongoni mwa wanachuoni wako waliosema kuwa makafiri hawatofanyiwa hesabu kwa sababu hawana hesabu yoyote. Si vyengine isipokuwa watapelekwa Motoni peke yake kwa sababu hawana hesabu yoyote. Wako wengine waliosema kuwa watafanyiwa hesabu ya kuthibitisha matendo yao, ukafiri na ukanajimungu wao. Baada ya hapo wapelekwe Motoni.

Mizani ni kifaa kinachopimia matendo ya waja ambapo mema yatawekwa kwenye sahani moja na maovu yatawekwa kwenye sahani jengine. Amesema (Ta´ala):

فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ

“Basi yule ambaye mizani yake itakuwa nzito, hao ndio wenye kufaulu, na yule ambaye mizani yake itakuwa mepesi, basi hao ndio ambao wamekhasirika nafsi zao.”[5]

Maovu yatapokuwa na uzito zaidi basi mtu atapata khasara na mema yatapokuwa na uzito zaidi basi mtu atapata faida. Huku ndio kupimwa kwa matendo.

Vivyo hivo yule ambaye atapokea kitabu chake kwa mkono wa kuume. Yule ambaye atapewa kitabu chake kwa mkono wa kushoto hesabu yake itakuwa ngumu na ataziona hali za khatari nzito na khatari baada ya khatari katika uwanja wa siku ya Qiyaamah, hesabu na sehemu ya mkusanyiko. Haya ni mambo makubwa endapo mtu atayafikiria.

[1] 53:31

[2] al-Bukhaariy (5705) na Muslim (218).

[3] 84:07-08

[4] al-Bukhaariy (103) na Muslim (2876).

[5] 23:102-103

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 182-284
  • Imechapishwa: 17/02/2021