143. Miongoni mwa dalili kwamba Allaah atawafufua viumbe baada ya kufa IX


Miongoni mwa dalili za kufufuliwa ni kutumia dalili za kuumbwa mbingu na ardhi. Ambaye ameweza kuwaumba viumbe hawa wakubwa ni muweza wa kumrudisha mwanadamu. Kwa sababu ambaye ameweza kitu kikubwa ana haki zaidi ya kilicho chini yake. Amesema (Ta´ala):

أَوَلَيْسَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَن يَخْلُقَ مِثْلَهُم ۚ بَلَىٰ وَهُوَ الْخَلَّاقُ الْعَلِيمُ

”Je, kwani Yule ambaye kaumba mbingu na ardhi hana uwezo wa kuumba mfano wavyo? Hapana shaka, Naye ni Mwingi wa kuumba, mjuzi wa kila jambo.”[1]

لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ

”Bila shaka uumbaji wa mbingu na ardhi ni mkubwa zaidi kuliko uumbaji wa watu, lakini watu wengi hawajui.”[2]

Hizi ni miongoni mwa dalili za kufufuliwa zinazothibitisha kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) atawafufua waliyomo ndani ya makaburi na kwamba atamlipa kila mtendaji  kwa matendo yake. Yakiwa ni mema atalipwa mema na yakiwa ni shari atalipwa shari. Akufuru mwenye kukufuru, afanye ufuska fasiki, zandiki na mkanamungu. Lakini watambue kuwa mbele yao kuna jambo la kufufuliwa, kukusanywa na kufanyiwa hesabu. Kuhusu muumini mwenye kumcha Allaah na ambaye anamwabudu Allaah na anajikurubisha kwa Allaah matendo yake hayatopotea. Ipo siku ambayo Allaah atamlipa kwa matendo yake, atampa malipo maradufu na atampa yale ambayo hakuwa anayafikiria na kuyatarajia.

[1] 36:81

[2] 40:57

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 182
  • Imechapishwa: 17/02/2021