142. Wale wenye kuonelea kwamba Shari´ah haiendani na zama hizi

Vivyo hivyo wanaingia katika kichenguzi hichi wale wanaosema kuwa Shari´ah ilikuwa inatumika katika zile zama za kale. Ama wakati wa sasa Shari´ah haiendani. Haya ni mambo ya kale yanayoendana na zama za kale, ama sasa maendeleo yamekuwa mengi na kuna vitu vipya vingi. Hii ina maana kuwa Shari´ah ni pungufu na kwamba haitoki kwa Mwingi wa hekima na Mwenye kustahiki kuhimidiwa. Hapana shaka yoyote ya ukafiri wa mwenye kusema maneno haya. Hili linaingia katika yule mwenye kudai kwamba inafaa kwa mtu kutoka katika Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba Shari´ah haiendani na zama hizi na kwamba eti inaendana tu na zama za kale. Ni wengi walioje wanaosema maneno haya! Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hautofaulu mwisho wa Ummah huu isipokuwa kwa yale yaliyofanya wakafaulu wa mwanzo wao.”[1]

Yaliyofanya wakafaulu wa mwanzo wao ni Qur-aan na Sunnah. Hivyo hautofaulu mwisho wa Ummah huu isipokuwa kwa Qur-aan na Sunnah. Kwa hivyo Qur-aan na Sunnah na Shari´ah ya Uislamu vinasilihi katika kila zama na mahali mpaka kisimame Qiyaamah. Isituhumiwe kwa mapungufu au kusema kwamba eti ni mambo madogomadogo. Kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amehukumu kuwa ni kamilifu. Amesema (Ta´ala):

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

”Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.” (al-Maaidah 05:03)

Hakufa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa ameiacha dini ni kamilifu na yenye kutumika katika kila zama na mahali. Miongoni mwa ukamilifu wake ni kwamba inasilihi katika kila zama na mahali. Ingelikuwa inaendana na zama fulani tofauti na zama zengine, isingelikuwa kamilifu. Bali ingelikuwa pungufu. Allaah ameshuhudia kwamba ni kamilifu. Upande mwingine watu hawa wanasema kuwa haiendani na zama hizi.

[1]Athar hii kaipokea Ibn ´Abdul-Barr katika “Tamhiyd” (15/292).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 183
  • Imechapishwa: 11/03/2019