141. Wenye kuonelea kwamba dalili za Qur-aan na Sunnah ni za kidhana

Kadhalika wanachuoni wa wanafalsafa na wanachuoni wa mantiki wana fungu katika haya; ambao wanasema kuwa dalili za Qur-aan na Sunnah zinafidisha dhana. Ama dalili za kiakili ni za yakini na zinafidisha yakini. Kwa ajili hii inapokuja katika ´Aqiydah hawategemei dalili za Qur-aan na Sunnah kwa sababu wanaona kuwa ni dalili zenye kutia dhana. Ama dalili za falsafa na mantiki dalili za yakini. Kwa ajili hiyo ndio maana mtaona ´Aqiydah yao imejengwa juu ya falsafa, ubishi na elimu ya mantiki. Hawatumii dalili kwa Aayah wala Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Huku ni kutoka katika Shari´ah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika jambo ambalo ni muhimu zaidi ambalo ni ´Aqiydah.

Jambo ambalo ni wajibu kwa muislamu ni kufuata Qur-aan na Sunnah katika mambo yote; katika adabu, ´Aqiydah, biashara, tabia na mambo mengine yote. Kwa sababu ujumbe wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni wenye kuenea na ni wenye kusilihi katika kila zama na mahali mpaka hapo Qiyaamah kitaposimama. Kwa sababu yule ambaye Kaiteremsha ni Mwingi wa hekima na Mjuzi wa kila kitu ambaye anajua yanayoendana na waja Wake katika kila zama mpaka hapo Qiyaamah kitaposimama. Ni Uteremsho uliyoteremshwa kutoka kwa Mwingi wa hekima, Mwenye kustahiki kuhimidiwa. Amesema (Ta´ala):

وَإِنَّهُ لَكِتَابٌ عَزِيزٌلَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ ۖتَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ

”Hakika hicho ni Kitabu kitukufu, haitokifikia batili mbele yake na wala nyuma yake – ni Uteremsho kutoka kwa Mwingi wa hekima, Mwenye kustahiki kuhimidiwa.” (al-Fuswswilat 41-42)

Imeenea na inaendana na katika kila zama na mahali. Hakuna muislamu yeyote awezaye kutoka ndani yake.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 182-183
  • Imechapishwa: 11/03/2019