05. Shaam ndio kuna uokozi wakati wa mtihani

29- ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Niliona kama nguzo ya Kitabu inavutwa kutoka chini ya mto wangu. Nikaiandama kwa macho na kuona kuwa ni nuru yenye kuangaza inayopelekwa kuelekea Shaam. Pindi kutapotokea mtihani imani itakuwa Shaam.”

Ameipokea al-Haakim aliyesema:

“Ni Swahiyh kwa masharti ya al-Bukhaariy na Muslim.”

30- Ka´b-ul-Ahbaar amesema:

“Ni katika ule wakati ambao moto utatokea Yemen na kuwafukuza watu kwenda Shaam. Watakaposafirishwa asubuhi, nao unasafiri. Watakapoenda, nao unaenda. Mtaposikia khabari zake, tokeni mwende Shaam.”

31- at-Tirmidhiy amepokea ya kwamba mtumwa wa Ibn ´Umar alimjia na kumwambia:

“Mambo yamenikuia magumu siku hizi. Nataka kuhamia Iraq.” Akasema: “Nenda Shaam, sehemu ya Mkusanyiko.”

32- Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

وَنَجَّيْنَاهُ وَلُوطًا إِلَى الْأَرْضِ الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا لِلْعَالَمِينَ

“Tukamuokoa na Luutw kuelekea ardhi ambayo Tumeibariki humo kwa walimwengu.”[1]

Qataadah amesema:

“Allaah aliwaokoa kuelekea Shaam, mahali pa mkusanyiko na pa kufufuliwa. Huko ndiko watakusanyika watu. Huko ndiko atateremka ´Iysaa bin Maryam (´alayhis-Swalaatu was-Salaam). Huko ndiko Allaah atamuua al-Masiyh mwongo.”

33- Ibn Shawdhab amesema:

“Tulikuwa tukiongelea Shaam. Nikamwambia Abu Sahl: “Hukufikiwa na khabari ya kwamba huko kutatokea hili na lile?” Akajibu: “Ndio, lakini yatayotokea huko ni afadhali kuliko yatayotokea sehemu zengine.”

34- ´Abdullaah bin Hawaalah amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mambo yataishilia maaskari watakuwa ni wenye kushikamana: wanajeshi wa Shaam, wanajeshi wa Yemen na wanajeshi wa Iraq.” Ibn Hawaalah akasema: ”Nijiunge na kina nani, ee Mtume wa Allaah, endapo nitakutana na hayo?” Akasema: ”Shikamana na Shaam kwani hakika ndio ardhi bora ya Allaah.” Huko Allaah huwateua waja Wake bora. Iwapo mtakataa basi chagueni Yemen na kunyweni kutoka chemchem yake. Hakika Allaah amechukua jukumu juu yangu la kuiangalia Shaam na watu wake.”

Ameipokea Imaam Ahmad, Abu Daawuud, Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh” yake na al-Haakim ambaye amesema:

”Mlolongo wa wapokezi wake ni Swahiyh.”

Abu Haatim ar-Raaziy amesema:

“Hadiyth ni Swahiyh, nzuri na geni.”

Imepokelewa kwa njia nyingi. Nimezitaja katika “Sharh at-Tirmidhiy”.

Wakati Abu Idriys al-Khawlaaniy alipokuwa akiielezea Hadiyth hii huongeza:

“Yule mwenye kuangaliwa na Allaah hapotei.”

Imepokelewa ya kwamba ´Abdullaah bin Hawaalah alikuwa akisema hivo hivyo.

[1] 21:71

  • Mhusika: Imaam ´Abdur-Rahmaan bin Rajab al-Baghdaadiy al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaa-il-ush-Shaam, uk. 43-46
  • Imechapishwa: 02/02/2017