19- Ndugu wa maiti pindi wanapofikiwa na khabari za kifo yanawalazimu mambo mawili:

La kwanza: Kufanya subira na kuridhia makadirio. Amesema (Ta´ala):

وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao [katika kazi zenu]. Wabashirie wale wenye kusubiri ambao unapowafika msiba basi husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea – hao zitakuwa juu yao baraka kutoka kwa Mola wao na rehema na hao ndio wenye kuongoka.”[1]

Pia kutokana na Hadiyth ya Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimpitia mwanamke aliyekuwa karibu na kaburi ambaye alikuwa analia ambapo akamwambia: “Mche Allaah na subiri!” Mwanamke yule akasema: “Nitokee mbali. Hakika wewe hufikwa na msiba uliyonifika.” Anas anasema: “Hakumjua.” Akaambiwa: “Ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Akapatwa na mfano wa kifo. Akaenda mpaka kwenye mlango wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hakuona mbele yake walinzi. Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hakika mimi sikukujua.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Hakika subira inakuwa katika ule mpigo wa kwanza.”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/115-116), Muslim (03/40-41), al-Bayhaqiy (04/65) na mtiririko ni wake.

Kusubiri kwa sababu ya kufiliwa na watoto kuna ujira mkubwa. Kumepokelewa kuhusu hilo Hadiyth nyingi. Nitataja baadhi yake:

1- “Hakuna muislamu yeyote anayefiwa na watoto watatu akaguswa na Moto isipokuwa ni kule kuhalalisha kiapo.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim, al-Bayhaqiy (04/67) kutoka kwa Abu Hurayrah.

2- “Hakuna waislamu wowote ambao watafiwa na watoto watatu ambao bado hawajabeleghe isipokuwa Allaah atawaingiza wazazi wake Peponi kwa sababu ya fadhilah za rehema Yake. Watakuwa mbele ya mlango miongoni mwa milango ya Peponi ambapo wataambiwa: “Ingieni Peponi!” Waseme: “Mpaka waje wazazi wetu.” Waambiwe: “Ingieni Peponi nyinyi na wazazi wenu kwa fadhilah za huruma ya Allaah.”

Ameipokea  an-Nasaa´iy (01/265), al-Bayhaqiy (04/68) na wengineo kutoka kwa Abu Hurayrah. Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim.

3- “Hakuna mwanamke yeyote atayefiwa na watoto watatu isipokuwa watakuwa ni kizuizi chake cha Moto.” Mwanamke mmoja akasema: “Na mwenye watoto wawili?” Akasema: “Na mwenye watoto wawili.”

Ameipokea al-Bukhaariy (03/94), Muslim na al-Bayhaqiy (04/67) kutoka kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh).

4- “Hakika Allaah haridhii kwa mja Wake aliyemwondolea kipenzi chake katika watu wa ardhini ambapo akasubiri na akatarajia thawabu zaidi ya Pepo.”

Ameipokea an-Nasaa´iy (01/264) kutoka kwa Abu ´Abdullaah bin ´Amr kwa cheni ya wapokezi nzuri.

La pili: Miongoni mwa mambo ambayo ni lazima kwa wale ndugu wa maiti ni al-Istirjaa´. Nako ni kule kusema: “Sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea”, kama ilivyokuja katika Aayah mbili zilizotangulia. Kisha azidishe kusema:

اللهم اجرني في مصيبتي وأخلف لي خيرا منها

“Ee Allaah! Nilipe kwa msiba wangu na Unipe badala bora kuliko nilichopoteza.”

Hayo ni kutokana na Hadiyth ya Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hakuna muislamu yeyote anayefikwa na msiba akasema yale aliyomwamrisha Allaah: “Sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea. Ee Allaah! Nilipe kwa msiba wangu na Unipe badala bora kuliko nilichopoteza” isipokuwa Allaah atampa badala bora kuliko alichopoteza.”

Umm Salamah anaendelea kusimulia:

“Wakati alipokufa Abu Salamah nilijiuliza nafsi yangu mwenyewe: “Ni muislamu yupi ambaye ni bora kuliko Abu Salamah?” Ni mtu wa kwanza mwenye nyumba ambaye alihajiri kwenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini nikayasema na Allaah akamnipa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinitumia Haatwib bin Abiy Balta´ah anipose kwa ajili yake. Nikasema: “Mimi nina msichana na nina wivu.” Akasema: “Kuhusu msichana wako nitamuomba Allaah amtosheleze kutokamana na yeye na nitamuomba Allaah amwondoshee wivu.”

Ameipokea Muslim (03/37), al-Bayhaqiy (04/65) na Ahmad (06/309).

[1] 02:155-157

[2] Imaam al-Baghawiy amesema:

”Anakusudia: isipokuwa  kwa yale makadirio ya Allaah kukitakasa kiapo chake. Nayo ni yale maneno Yake (´Azza wa Jall):

وَإِن مِّنكُمْ إِلَّا وَارِدُهَا

“Hakuna yeyote miongoni mwenu isipokuwa ni mwenye kuufikia [huo Moto]. (19:71)

Atapopita na kuuvuka [huo Moto] kiapo Chake kitakuwa kimetakasika.”  Sharh-us-Sunnah (05/451).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 33-35
  • Imechapishwa: 31/12/2019