14. Usiku wa Qadar


Usiku wa Qadar ndio usiku bora kabisa. Ndani yake Allaah ameteremsha Qur-aan. Ameeleza (Subhaanah) ya kwamba ni usiku ulio bora kuliko miezi elfu moja na umebarikiwa na kwamba ndani yake kunabainishwa kila jambo la hekima. Allaah (Subhaanah) amesema mwanzoni mwa Suurah “ad-Dukhaan”:

حم وَالْكِتَابِ الْمُبِينِ إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ أَمْرًا مِّنْ عِندِنَا ۚ إِنَّا كُنَّا مُرْسِلِينَ رَحْمَةً مِّن رَّبِّكَ ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ

“Haa Miym. Napaa kwa Kitabu kinachobainisha! Hakika Sisi tumeiteremsha katika usiku uliobarikiwa – hakika Sisi tumekuwa [daima ni] wenye kuonya [watu] – Humo [katika usiku huo] hupambanuliwa kila jambo la hikmah na jambo [Tunalokadiria ni lenye] kutoka Kwetu – hakika Sisi [daima] ndio wenye kutuma [wajumbe Wetu kwa mafunzo na mwongozo]. – Ni Rahmah kutoka kwa Mola wako, hakika Yeye ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote.”[1]

Allaah (Subhaanah) amesema:

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ

“Hakika Sisi Tumeiteremsha katika usiku wa Qadar. Na nini kitakachokujulisha ni nini huo usiku wa Qadar? Usiku wa cheo ni mbora kuliko miezi elfu; wanateremka humo Malaika na Roho kwa idhini ya Mola wao kwa [ajili ya kutekeleza] kila jambo [Lake]. [Usiku huo kunakuwa na] amani mpaka kuchomoza alfajiri!”[2]

Imesihi ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayesimama usiku wa Qadar kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[3]

Kusimama kunajumuishwa swalah, Adhkaar, du´aa, kusoma Qur-aan na matendo mengine ya kheri. Suurah hii imefahamisha kuwa matendo mema ndani yake ni bora kuliko matendo ya miezi elfu moja. Hii ni fadhila kubwa na rehema za Allaah kwa waja Wake.

Inampasa kila muislamu kuuadhimisha na kuutumia kwa ´ibaadah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuwa unakuwa katika yale masiku kumi ya mwisho ya Ramadhaan na kwamba uwezekano mkubwa ni kuutafuta katika yale masiku ya witiri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Utafuteni katika yale masiku kumi ya mwisho ya Ramadhaan na utafuteni katika kila usiku wa witiri.”[4]

Hadiyth hizi Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zinafahamisha ya kwamba usiku huu unaweza kupatikana usiku wowote katika yale masiku kumi ya mwisho. Usiku wa Qadar haupatikani kila mwaka usiku mmoja. Unaweza kupatikana tarehe 21, 23, 25, 27 au 29. Unaweza vilevile kupatikana katika masiku ya kawaida.

Atayesimama zile nyusiku zote kumi kwa imani na kwa matarajio haina shaka kuwa atakutana na usiku huu na amefuzu kwa kile alichoahidi Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijitahidi zaidi katika masiku haya. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijitahidi zaidi katika yale masiku kumi ya mwisho kuliko anavyojitahidi masiku mengine.”[5]

Amesema vilevile:

“Yalipokuwa yakiingia yale masiku kumi anaamka usiku na kuamsha vilevile familia yake, akifanya bidii na akifunga vizuri kikoi chake.”[6]

Mara alikuwa akiyatumia masiku kumi haya akifanya I´tikaaf. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ

“Hakika mna kigezo kizuri kwa Mtume wa Allaah.”[7]

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aseme nini iwapo atakutana na usiku wa Qadar. Akasema:

“Sema: “Allaah! Hakika Wewe ni msamehevu unayependa kusamehe. Nisamehe.””[8]

Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Salaf waliokuja baada yao walikuwa wakijitahidi katika masiku kumi haya ya mwisho na wakijibidisha kwa matendo mema.

Ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwa waislamu wote kumuiga Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake watukufu (Radhiya Allaahu ´anhum) na Salaf wa Ummah huu. Kwa hiyo wanatakiwa kuyatumia masiku haya kwa kuswali, kusoma Qur-aan na kuomba du´aa na kufanya aina mbalimbali za ´ibaadah kwa imani na kwa kutarajia malipo ili madhambi yao yasamehewe na waokolewe kutokamana na Moto. Ni fadhila, tunuku na ukarimu kutoka Kwake (Subhaanah). Qur-aan na Sunnah vimefahamisha kuwa ahadi hii kuu ni uhalisia endapo kutaepukwa madhambi makubwa. Allaah (Subhaanah) amesema:

إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُم مُّدْخَلًا كَرِيمًا

“Mkijiepusha madhambi makubwa mnayokatazwa Tutakufutieni madhambi yenu madogo na Tutakuingizeni katika mahali patukufu.”[9]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah tano, Ijumaa mpaka Ijumaa na Ramadhaan mpaka Ramadhaan vinafuta vilivyo kati yavyo endapo kutaepukwa madhambi makubwa.”[10]

Ee waislamu! Swawm ni kitendo chema na kikubwa na thawabu zake ni tele na khaswa khaswa swawm ya Ramadhaan. Uadhimisheni – Allaah akurehemuni – kwa kuwa na nia njema na kujitahidi kuhifadhi swawm yake, kusimama nyusiku zake na kukimbilia matendo mema na kutubia madhambi na makosa yote. Tahadharini na yale Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walokataza na mtiini katika Ramadhaan na wakati mwingine. Usianeni na saidianeni juu ya hayo. Amrisheni mema na katazeni maovu ili muweze kupata Pepo, furaha, utukufu na kufuzu duniani na Aakhirah.

Tunamuomba Allaah atukinge sisi, nyinyi na waislamu wengine wote kutokamana na yale yenye kusababisha ghadhabu Zake na atukubalie sote swawm na visimamo vyetu, awatengeneze watawala wa waislamu na ainusuru dini kupitia Wao na awakoseshe nusura maadui Wake kupitia wao na awawafikishe wote kuweza kuifahamu dini na kuwa na msimamo juu yake na kuhukumu na kuhukumiwa kwayo katika mambo yote. Hakika Yeye juu ya kila kitu ni muweza.

Swalah na salaam zimwendee mja na Mtume Wake, Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake.

[1] 44:01-06

[2] 97:01-05

[3] al-Bukhaariy (1901) na Muslim (760).

[4] al-Bukhaariy (2021) na Muslim (1165).

[5] Muslim (1175).

[6] al-Bukhaariy (2024) na Muslim (1174).

[7] 33:21

[8] at-Tirmidhiy (3513), Ibn Maajah (3850) na Ahmad (25423). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (4423).

[9] 04:31

[10] Muslim (2339).