14. Ulazima wa kuamini ngazi nne za Qadar


Qadar ina ngazi nne ambazo ni lazima kuziamini zote:

Ngazi ya kwanza: Kuamini kwamba Allaah alikijua kila kitu kwa ujuzi Wake wa milele ambayo anasifika kwayo milele na siku zote. Ngazi hii ndio waliyoipinga Qadariyyah waliochupa mpaka.

Ngazi ya pili: Kuamini kwamba Allaah ameandika katika Ubao uliohifadhiwa kila kitu. Hayo ni kutokana na Hadiyth:

“Kitu cha kwanza alichoumba Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ni kalamu. Kisha akaiambia: “Andika!” Ikasema: “Niandike nini?” Akasema: “Andika yatayokuwa na yatayokuweko mpaka Qiyaamah kisimame.”[1]

Allaah (Jalla wa ´Alaa) anasema:

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ

“Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa upo katika Kitabu… “

Kitabu ni Ubao uliohifadhiwa.

مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا

“… kabla hatujautokezesha.”

Bi maana kabla ya kuumba.

إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.”[2]

Uandikaji:

“Kabla ya kuumba mbingu na ardhi kwa miaka 50.000 na ´Arhi Yake ilikuwa juu ya maji.”

Uandikaji ulitangulia kitambo kabla ya kuumbwa mbingu na ardhi.

Ngazi ya tatu: Matakwa na utashi: Kila kitu kinachotokea ni kwa kutaka kwa Allaah. Hapa kuna Radd kwa Qadariyyah. Hakukuwi katika ufalme Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) yale asiyoyataka Allaah:

وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا اقْتَتَلُوا وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ

“Lau angelitaka Allaah wasingelipigana lakini Allaah anafanya atakavyo.”[3]

إِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يَشَاءُ

“Hakika Allaah anafanya atakavyo.”[4]

Kila kitu kinachotokea Allaah amekitaka baada ya kukijua na kukiandika katika Ubao uliohifadhiwa.

Ngazi ya nne: Uumbaji: Amekijua, akakiandika na akakikuumba (Subhaanahu wa Ta´ala).

Ni lazima uamini ngazi zote hizi. Vinginevyo utakuwa si mwenye kuamini mipango na makadirio ya Allaah.

[1] Abu Daawuud (4700), at-Tirmidhiy (2155, 3319), Ahmad katika ”al-Musnad” (05/317, nambari. 22705, 22707) kupitia kwa ´Ubaadah bin as-Swaamitw (Radhiya Allaahu ´anh).

[2] 57:22

[3] 02:253

[4] 22:18

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 32-33
  • Imechapishwa: 08/03/2021