14. Ufikaji wa al-Madiynah


Answaar walipata khabari ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameiacha Makkah na wanawaendea. Kila siku walikuwa wakitoka na kwenda kwenye jua ili kumsubiri. Jumatatu Rabbiy´ al-Awwal miaka kumi na tatu baada ya utume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akafika wakati wa asubuhi. Answaar walikuwa wameshatoka nje siku hiyo. Baada ya kusimama na kumsubiri kwa muda mrefu wakarejea majumbani kwao. Mtu wa kwanza kumuona alikuwa ni myahudi ambaye alikuwa amesimama kwenye paa ya nyumba. Akapiga kelele kwa sauti ya juu:

“Ee Banuu Qaylah! Babu yenu mliyekuwa mnamsubiri amekuja!”

Answaar wakatoka na silaha zao na wakamsalimia kwa salaam ya utume. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatua Qubaa´ kwa Kulthum bin al-Hadam. Maoni mengine yanasema ilikuwa kwa Sa´d bin Khaythamah. Waislamu wakaja kumsalimia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wengi wao walikuwa bado hawajamuona hapo kabla. Baadhi yao, au wengi wao, walikuwa wanafikiria kuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Abu Bakr kwa sababu ya mvi zake nyingi. Wakati joto lilizidi kuwa kali Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) akachukua kitambaa ili kumkinga na jua Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hapo ndipo watu wakajua Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni nani.

  • Mhusika: Imaam Ismaa´iyl bin Kathiyr ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fusuwl fiy Siyrat-ir-Rasuwl, uk. 37-38
  • Imechapishwa: 18/03/2017