14. Sunnah pekee ndio yenye kuleta umoja kwa waislamu

Kutokana na yaliyobainishwa hapo mwanzoni umetambua kuwa Sunnah ni kuswali swalah za ´Iyd mahali pa uwanja na ni jambo ambalo maimamu wamekubaliana juu yake kutoka katika mtazamo wa kielimu. Vilevile kufanya hilo mahali pa uwanja kunapelekea katika faida na hekima nyingi ambazo hazipatikani kwenye misikiti mingi. Ndio maana inatakiwa kwa waislamu kurudi katika Sunnah ya Mtume wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kushirikiana na wale ambao wanapupia kuihuisha Sunnah hii katika miji hii. Hakika mkono wa Allaah uko juu ya kundi linalofuata Sunnah na sio kundi linaloenda kinyume nayo!

Haimstahikii mwenye busara kusema kwamba kuihuisha Sunnah hii kunapelekea kuwafarikisha waislamu, kwa sababu wakiswali katika misikiti yao makundi kwa makundi, kuswali mahali pa uwanja ina maana ya kwamba watatakiwa waiache na hivyo basi itakuwa ni kuzua makundi mapya – jambo tusilohitajia. Tuna haja ya kuyapunguza makundi, na sio kuyaongeza.

Haimpasi muislamu aliye na busara kusema maneno kama haya, kwa sababu yanapelekea katika matukio mabaya ambayo haiwezi kufikiriwa kuwa muumini anaweza kuyakusudia. Kwa maneno haya inapata kufahamika kuwa kuitendea kazi Sunnah na maoni waliokubaliana kwayo maimamu wote, jambo ambalo tumelibainisha kwa ufafanuzi, ni kuwafarikisha waislamu na kutawanyisha mkusanyiko wao. Kule kuyafikiria tu maneno haya kunatosheleza kubatilisha maneno haya. Uhakika wa mambo ni kwamba tunaona kuwa njia itayowafanya waislamu kuwa kitu kimoja ni pale wataporejea katika Sunnah. Hili ndilo tunamuabudu Allaah kwalo. Hili khaswa ile Sunnah ya kimatendo iliokuwa ikifanywa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika maisha yake yote na akauacha juu yake Ummah wake na wengine waliokuja baada yake.

Ikiwa unataka kupata mfano wa karibu, basi inakutosheleza hali tuliyomo ya kuswali mahali penye uwanja. Waislamu leo wamefarikiana juu ya swalah hii na kugawanyika katika makundi mengi tofauti na Sunnah. Ikiwa tunataka kuwafanya wawe kitu kimoja, hatuna njia nyingine isipokuwa kutoka katika ardhi pana itayowakusanya waislamu wote wanawake kwa wanaume. Wafanye sehemu hii kuwa uwanja wa kuswalia na watekeleze hapo ´ibaadah hii kubwa, ambayo ni swalah ya ´Iyd. Haya ndio yaliyoamrishwa na Sunnah. Vipi basi mtu anaweza kusema kuwa kuitendea kazi Sunnah hii kunafarikisha umoja wa waislamu!

Ndio, ni kweli ya kwamba kuihuisha Sunnah hii ina maana ya kwamba itapelekea kuunda mkusanyiko mpya na kuachana na ile mikusanyiko mingine iliyotawanyika inayofanyika kwenye misikiti mingi. Lakini pindi ilipokuwa makusudio ya mkusanyiko huu mpya ni kutaka kuikusanya mikusanyiko yote katika mkusanyiko mmoja, kama mambo yalivokuwa katika zama zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na katika zama za makhaliyfah waongofu, ndipo ikalazimika kupatikana kwa mkusanyiko huu. Kwa sababu mkusanyiko mmoja hauwi kwa mara moja kama ambavyo hauwi pasi na wao. Isitoshe kuna msingi unaosema kwamba yale mambo ambayo yanahitajika ili kutekeleza jambo la wajibu basi nayo yatakuwa ni wajibu. Hili linazidi kuthibitisha zaidi utambuzi ya kwamba kuna udharurah wa kupatikana mkusanyiko mmoja huu, kwa sababu uko juu ya Sunnah ambayo malengo yake ni kuhakikisha mkusanyiko huu kwa maana yake pana tofauti na ile mikusanyiko mingine yote.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swalaat-ul-´Iydayn, uk. 43-45
  • Imechapishwa: 13/05/2020