15. Anayefanyia dhihaka dini au jambo la kidini

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

06 – Mwenye kufanyia istihizai kitu katika dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), thawabu au adhabu ya Allaah, basi amekufuru. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema: “Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake? Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu”.”[1]

MAELEZO

Miongoni mwa vichenguzi vya Uislamu ni yule ambaye anafanyia mzaha kitu miongoni mwa yale mambo aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akakichezea shere kitu katika dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), thawabu au adhabu yake, basi anakufuru. Akifanyia mzaha swalah amekufuru. Akifanyia mzaha zakaah amekufuru. Akifanyia mzaha swawm amekufuru. Akiwafanyia mzaha waswaliji, kama kuifanyia maskhara swalah ambayo wanaiswali waislamu, amekufuru. Kadhalika akifanyia mzaha ndevu kwa sababu ya kuchukia yale maamrisho yaliyoletwa na Uislamu juu ya kufuga ndevu anakufuru. Kwa sababu ni jambo limewekwa na Allaah kupitia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini ikiwa anamfanyia maskhara mtu yeye kama yeye, hakufuru.

Vivyo hivyo akiichezea shere Pepo na Moto. Pepo ni malipo kwa waumini na Moto ni adhabu kwa makafiri. Akivichezea shere na istihizai na akahoji viwili hivyo kwa njia ya dhihaka, basi anakufuru. Vilevile inahusiana na yule mwenye kufanyia istihizai thawabu za matendo mema, kwa mfano mtu mwenye kusikia au kusoma Hadiyth iliyosimuliwa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kusema:

سُبْحَانَ اللَّهِ وَبِحَمْدِهِ

“Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu na himdi zote ni Zake.”

kwa siku mara mia moja anafutiwa makosa yake hata kama yatakuwa ni mfano wa povu la bahari.”[2]

Mtu akazifanyia thawabu hizi mzaha na maskhara – na si kwa sababu haonelei kuwa ni Swahiyh – anakufuru. Akifanyia dhihaka chochote katika dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), thawabu ambazo Allaah amewaandalia wenye kutii, thawabu ambazo Allaah ameziandaa kwa ajili ya matendo mem, adhabu ambayo Allaah amewaandalia watenda madhambi au amemwaandalia kafiri, basi anakufuru. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema: “Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake? Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu”.”

Amewathibitishia ukafiri baada ya kuamini kwao. Aayah hii imeteremka juu ya kikosi cha wanafiki katika vita vya Tabuuk ambao walimfanyia dhihaka Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake wasomaji. Baadhi waliwaambia wengine:

“Hatujapatapo kuona mfano wa wasomaji wetu hawa; wana matumbo makubwa, wanasema uwongo sana na ni waoga wakati wa mapambano.”

Bi maana hawajawahi kuona watu mfano wao kwa kula, kusema uwongo sana na waoga wakati wa kupigana vita na maadui. Wanamaanisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake wasomaji. ´Awf bin Maalik akawasikia walipokuwa wanazungumza ambapo akawaambia:

“Umesema uwongo. Wewe ni mnafiki. Nitamweleza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Akaja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumweleza. Alipofika kwake akakuta Wahy umeshamtangulia. Allaah akateremsha Aayah ifuatayo:

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema: “Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake? Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu”.”

Akaja mtu yule aliyezungumza maneno haya na kutaka kutoa udhuru kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na huku akisema:

“Ee Mtume wa Allaah! Tulikuwa tunapiga porojo tu na kucheza.”

Bi maana hatufanya hivo kwa kukusudia. Tulizungumza vile kwa sababu tu ya kujifanyia wepesi urefu wa safari. Kama ambavyo baadhi yetu husema ya kwamba ni mazungumzo tu kujifanyia wepesi urefu wa safari. Anasema hivyo na huku Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hazidishi mbali na kusoma Aayah ifuatayo:

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema: “Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake? Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu”.”

Mtu huyo alikuwa ameshikilia kamba ya kipando cha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni ile kamba inayokuwa imezunguka kwenye kiuno cha ngamia na huku miguu yake inaburuza kwenye ardhi na mawe yanapiga miguu yake na wakati huohuo huku anazidi kuomba udhuru. Lakini pamoja na hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hazidishi mbali na kumsomea Aayah hii:

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema: “Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake? Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu”.”

Allaah akawathibitishia ukafiri baada ya kuamini kwao pale aliposema:

قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu”.”[3]

Ikiwa watu hawa walimchezea shere Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum), kwa maana nyingine walikejeli utu wao, na kusema kuwa watu hawa wanakula sana, kusema uwongo sana na ni waoga wakati wa mapambano, vipi kwa yule mwenye kufanyia dhihaka dini ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama mfano wa anayefanyia maskhara swalah, zakaah, swawm, Pepo, Moto, kufufuliwa, malipo, Njia na mizani? Anayefanyia mzaha kitu katika hayo basi anakufuru.

[1] 09:65-66

[2] al-Bukhaariy (6405) na Muslim (2691)

[3] 09:65-66. Kisa hiki kimepokelewa na Ibn Jariyr (Rahimahu Allaah) katika Tafsiyr yake (11/543)

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tabswiyr-ul-Anaam bisharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 37-40
  • Imechapishwa: 15/04/2023