14. Radd kwa wakanamungu, Baatwiniyyah na Suufiyyah

Miongoni mwa I´tiqaad za kikafiri zinazopingana na ´Aqiydah sahihi na yale waliyokuja nayo Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) ni pamoja na yale wanayoitakidi wakanamungu hii leo katika wafuasi wa Marx, Lenin na walinganizi wengineo wa ukanamungu na ukafiri. Ni mamoja wakayaita hayo ujamaa, ukomunisti, Ba´thiyyah na mengineyo. Hakika miongoni mwa misingi ya wakanamungu hawa ni pamoja vilevile na kuonelea kuwa hakuna mungu na kwamba kuna maisha haya tu ya kidunia. Miongoni mwa misingi yao vilevile ni pamoja na kukanusha kufufuliwa, Pepo na Moto na wanazikana dini zote. Atayajua hayo kiyakini yule atayesoma vitabu vyao na yale wanayoamini. Ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba I´tiqaad hii inapingana na dini zote za kimbingu. Hakika wenye nayo yatawapelekea katika matokeo mabaya duniani na Aakhirah.

Miongoni mwa I´tiqaad batili pia ni pamoja vilevile na yale wanayoitakidi baadhi ya Baatwiniyyah na Suufiyyah ya kwamba baadhi ya wale wanaowaita “mawalii” wanashirikiana na Allaah katika kuyaendesha mambo na wanashiriki pia katika kuendesha kazi za ulimwengu na wanawaita waungu wao “Aqtwaab”, “Awtaad”, “Aghwaath” na majina mengine waliyoyazusha wao wenyewe. Hii ni shirki mbaya kabisa katika uola wa Allaah. Shirki hii ni mbaya zaidi kuliko shirki ya kipindi cha kishirikina cha kiarabu. Washirikina wa kiarabu hawakushirikisha katika uola wa Allaah. Walishirikisha katika ´ibaadah. Isitoshe walikuwa wakishirikisha katika kipindi cha raha. Kuhusiana na kipindi cha shida walikuwa wakimtakasia ´ibaadah Allaah pekee. Allaah (Subhaanah) amesema:

فَإِذَا رَكِبُوا فِي الْفُلْكِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ إِذَا هُمْ يُشْرِكُونَ

“Wanapopanda merikebu humwomba Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini, lakini anapowaokoa katika nchikavu, tahamaki hao wanamshirikisha.” (29:65)

Walikuwa wakikubali kuwa Allaah pekee ndiye muumba. Amesema (Subhaanah):

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ

“Ukiwauliza: “Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi?” Basi watasema: “Allaah.” (31:25)

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ

“Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini au nani anayemiliki kusikia na kuona na nani anayemtoa aliye hai kutoka maiti na anayemtoa maiti kutoka aliye uhai na nani anayeendesha mambo yote? Watasema: “Ni Allaah”, basi sema: “Basi kwa nini hamchi?” (10:31)

Aayah zilizo na maana kama hii ni nyingi.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Marejeo: al-´Aqiydah as-Swahiyhah wa maa yudhwaadduhaa, uk. 12-13
  • Imechapishwa: 31/05/2023