14. Radd juu ya utata wa kwamba wanayofanya washirikina wamepangiwa na Allaah

Pili: Hoja walizotoa washirikina wa Quraysh na wengineo. Walikuwa wakitumia hoja kwa Qadar kwa ajili ya kutakasa shirki waliyokuwemo. Amesema (Ta´ala) katika Suurah “al-An´aam”:

سَيَقُولُ الَّذِينَ أَشْرَكُوا لَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا أَشْرَكْنَا وَلَا آبَاؤُنَا وَلَا حَرَّمْنَا مِن شَيْءٍ

“Watasema wale walioshirikisha: “Lau Allaah angelitaka tusingefanya shirki wala baba zetu pia na wala tusingeliharamisha chochote.”[1]

Vilevile amesema katika Suurah “an-Nahl”:

وَقَالَ الَّذِينَ أَشْرَكُوا لَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا عَبَدْنَا مِن دُونِهِ مِن شَيْءٍ نَّحْنُ وَلَا آبَاؤُنَا وَلَا حَرَّمْنَا مِن دُونِهِ مِن شَيْءٍ

“Wale washirikina wakasema: “Kama angelitaka Allaah tusingeliabudu chochote badala Yake – sisi wala baba zetu – wala tusingeliharamisha chochote pasi Naye.”[2]

Amesema katika Suurah “az-Zukhruf”:

وَقَالُوا لَوْ شَاءَ الرَّحْمَـٰنُ مَا عَبَدْنَاهُم

“Wakasema: “Angelitaka Mwingi wa huruma tusingeliyaabudu [waungu wa uongo].”[3]

Haafidhw Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah) amesema kwa mnasaba wa Aayah ya “al-An´aam:”

“Huu ni mjadala uliotajwa na Allaah (Ta´ala) na ni utata waliobabaisha kwao washirikina katika shirki zao na kuharamisha Aliyoharamisha: ya kwamba Allaah aliijua shirki wanayoifanya na kuharamisha Aliyoharamisha ilihali ni muweza wa kuyabadilisha kwa Yeye kuwatunuku imani na kuwazuia wao na shirki, lakini hata hivyo Hakufanya hivo. Hiyo ni dalili inayoonyesha kwamba ni kwa utashi, matakwa na kuwaridhia.”

Akaendelea kusema:

“Ni hoja  batilifu. Kwa sababu ingelikuwa ni kweli ni kwa nini Allaah awaadhibu, kuwatumilizia Mitume wake watukufu na awaonjeshe washirikina adhabu kali:

قُلْ هَلْ عِندَكُم مِّنْ عِلْمٍ

“Sema: “Je, mna elimu yoyote… “

Bi maana kwamba Allaah ni mwenye kuwaridhia kwa yale mliyomo?

فَتُخْرِجُوهُ لَنَا

“… mtutolee?”

Bi maana mtudhihirishie na kutuwekea wazi:

إِن تَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ

“Hakuna chengine mnachofuata isipokuwa dhana tu.”

Bi maana udanganyifu na mawazo:

إِن تَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ أَنتُمْ إِلَّا تَخْرُصُونَ

“Hakuna chengine mnachofuata isipokuwa dhana tu; nanyi si lolote isipokuwa mnabuni uongo.”

mnamkadhibisha Allaah katika yale mnayodai.”[4]

Vilevile amesema wakati wa kufasiri Aayah ya “an-Nahl”:

“Maneno yao yanalenga kwamba iwapo kweli Allaah (Ta´ala) anachukia kile tunachokifanya basi angelitukemea kwa kutuadhibu na asingetuwezesha kuyafanya. Allaah (Ta´ala) akasema hali ya kutaddi utata wao:

فَهَلْ عَلَى الرُّسُلِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ

“Kuna jengine juu ya Mtume isipokuwa ufikishaji wa wazi?”[5]

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ ۖ فَمِنْهُم مَّنْ هَدَى اللَّـهُ وَمِنْهُم مَّنْ حَقَّتْ عَلَيْهِ الضَّلَالَةُ ۚ فَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ

“Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut [waungu batili]. Basi miongoni mwao wako ambao Allaah amewahidi na miongoni mwao wako ambao umethibiti kwake upotevu. Basi tembeeni katika ardhi kisha mtazame vipi ilikuwa hatima ya wenye kukadhibisha.”[6]

Mambo hayako vile mnavodai ya kwamba Hakukaripieni. Bali Amekukameeni kwa makemeo makali. Akakukatazeni makatazo makali kabisa. Ametuma Mtume katika kila Ummah na katika kila karne na katika kila kundi la watu na wote hao wanalingania katika kumuabudu Allaah na wakati huohuo wanakataza kumuabudu mwingine asiyekuwa Allaah:

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume [alinganie] kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut.”[7]

Hakuacha (Ta´ala) kuwatumia watu Mtume juu ya jambo hilo tokea hapo kulipozuka shirki kwa wana wa Aadam. Kuanzia kwa watu wa Nuuh ambaye aliwatumilizia Nuuh, na ndiye alikuwa Mtume wa kwanza Allaah kumtumiliza kwa watu wa ardhini, mpaka kwa Mtume wa mwisho ambaye ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye ulinganizi wake unawahusu majini na watu, mashariki na magharibi mwa ardhi.”

Wote mambo yalivyo ni kama alivyosema Allaah (Ta´ala):

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi niabuduni.”[8]

Vilevile amesema (Ta´ala):

وَاسْأَلْ مَنْ أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رُّسُلِنَا أَجَعَلْنَا مِن دُونِ الرَّحْمَـٰنِ آلِهَةً يُعْبَدُونَ

“Waulize wale Tuliowatuma kabla yako miongoni mwa Mitume Wetu, je, tulifanya badala ya Mwingi wa huruma waungu wengine wakiabudiwa?”[9]

Amesema (Ta´ala) katika Aayah hii tukufu:

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume [alinganie] kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut.”[10]

Baada ya yote haya ni vipi basi itafaa kwa mshirikina yeyote aseme:

لَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا عَبَدْنَا مِن دُونِهِ مِن شَيْءٍ نَّحْنُ وَلَا آبَاؤُنَا وَلَا حَرَّمْنَا مِن دُونِهِ مِن شَيْءٍ

“Wale washirikina wakasema: “Kama angelitaka Allaah tusingeliabudu chochote badala Yake – sisi wala baba zetu – wala tusingeliharamisha chochote pasi Naye.”[11]

Matakwa ya Allaah (Ta´ala) ya Kishari´ah si yenye kuwagusa. Kwa sababu amewakataza kufanya hivo kupitia Mitume wake.

Kuhusu matakwa yao ya kilimwengu kwamba ndio yenye kuwawezesha kufanya hivo si hoja kwao.”

Akaendelea kusema:

“Halafu isitoshe (Ta´ala) amekhabarisha kwamba amewakemea kupitia adhabu aliyowapa [wengine] hapa duniani kupitia maonyo ya Mitume.”[12]

Walichokusudia kwa maneno yao haya ni kutoa udhuru kwa matendo yao mabaya. Kwani wao hawaoni matendo yao yalivyo mabaya. Bali wao:

يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا

“… na huku wao wakidhani kuwa wanapata mazuri kwa matendo yao.”[13]

Wao wanayaabudu masanamu ili yawakurubishe karibu na Allaah. Hakuna jengine walichokusudia isipokuwa kutumia hoja yale wayafanyayo kwamba ni haki na ni yenye kukubali mbele ya Allaah. Ndipo Allaah (Subhaanah) akawaraddi ya kwamba mambo yangelikuwa hivo wanavosema basi asingelituma Mitume kuja kuwakemea na asingeliwaadhibu.

[1] 06:148

[2] 16:36

[3] 43:20

[4] Tazama ”Tafsiyr-ul-Qur-aan al-´Adhwiym” (01/186) ya Ibn Kathiyr.

[5] 16:35

[6] 16:36

[7] 16:36

[8] 21:25

[9] 43:45

[10] 16:36

[11] 16:36

[12] Tazama ”Tafsiyr-ul-Qur-aan al-´Adhwiym” (01/586-587) ya Ibn Kathiyr.

[13] 18:104

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Haqiyqat-it-Tawhiyd, uk. 23-27
  • Imechapishwa: 27/03/2019