14. Ndio maana mlinganizi anatakiwa awe na subira

Kwa sababu ya kutofautiana kwa watu namna hii na kutofautiana misimamo yao ndio maana ni lazima kwa yule anayelingania katika elimu na kuitendea kazi awe na subira juu ya yale maudhi yanayomsibu. Kiigizo chake katika hilo ni Mitume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Kila mlinganizi anayelingania kwa Allaah anatakiwa kuwa ni mwenye subira, mwenye nia nzuri, akitarajia nyuma ya ulinganizi wake ridhaa ya Allaah na Pepo Yake na wakati huohuo anakhofia adhabu ya Allaah (Tabaarak  wa Ta´ala).

Ametumia (Rahimahu Allaah) dalili kwa Suurah kubwa ambayo ndani yake kuna ulinganizi katika elimu, kuitendea kazi, kuwalingania watu kwayo, kuwa na subira juu ya yale maudhi yanayomfika mtu katika njia hii. Nayo si nyingine ni Suurah “al-´Aswr” ambapo Allaah  (Tabaarak  wa Ta´ala) ametaja kanuni yenye kuenea kwamba kila mtu amekhasirika ikiwa na maana ameangamia. Isipokuwa wale aliowavua kwa kusema:

إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ

“… isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana kwa kufuata ya haki na wakausiana kuwa na subira.”[1]

Hawa ambao wamekusanya kati ya elimu, kuitendea kazi, kuwaita viumbe kwayo na kusubiri juu ya maudhi yanayomkumba mtu ndani yake, hawa ndio wafu wasafi kabisa, wabora wao na watakasifu wao. Ndio maana Allaah (Tabaarak  wa Ta´ala) akawavua kutoka miongoni mwa wakhasirikaji. Mwenye kusalimika kutoka khasarani ndio mwenye kufaulu na ndiye mwenye kufuzu kuliko kukubwa katika dunia yake, ndani ya maisha ya kaburini na Aakhirah. Kwa sababu yeye ndiye kateleza amri ya Mola Wake ambapo ameamini yale yote ambayo ni lazima kuyaamini kwa uinje na kwa undani, ya maneno, ya vitendo na ya kuamini. Isitohe akafanya matendo mema kwa viungo vya mwili wake kwa aina mbalimbali za ´ibaadah ambazo ndio kazi ya viungo vya mwili na hisia. Kisha wakaanza kuwalingania viumbe katika faida ya kikweli hali ya kuwaamrisha, kuwakataza, kuwawekea wazi, kuwabainishia, kuwanasihi na kuwachunga – anafanya yote hayo pasi na kutaka kutoka kwao malipo wala shukurani. Lakini anachotaka kutoka kwao wapite juu ya radhi za Mola Wao, wajikurubishe Kwake kwa matendo mema, wajiepushe na sehemu za utelezi. Watu aina hii ndio wenye kuridhiwa na Allaah (Tabaarak  wa Ta´ala) na atawatunuku Pepo Yake ambayo amewaahidi wapenzi Wake na kundi Lake lililofaulu. Watu hawa wamesubiri juu ya hayo subira yenye kuendelea kwenye maisha yao yote ambayo wamewalingania viumbe kwa Allaah (Tabaarak  wa Ta´ala).

[1] 103 : 01-03

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Twariyqal-Usuwl ilaa idhwaah-ith-Thalaat-il-Usuwl, uk. 32-33
  • Imechapishwa: 24/11/2021