14. Ndio maana Mitume wakatumilizwa

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume [awaamrishe watu wake] kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut!”[1]

MAELEZO

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) anaeleza kwamba ametumiliza katika kila Ummah Mtume. Ummah maana yake ni kundi, kizazi na pote la watu.

Mtume ni mtu ambaye ameteremshiwa Shari´ah na akaamrishwa kuifikisha. Mitume ni wengi na baadhi yao wametajwa na Allaah ndani ya Qur-aan:

وَرُسُلًا قَدْ قَصَصْنَاهُمْ عَلَيْكَ مِن قَبْلُ وَرُسُلًا لَّمْ نَقْصُصْهُمْ عَلَيْكَ ۚ وَكَلَّمَ اللَّـهُ مُوسَىٰ تَكْلِيمًا

“Mitume  Tuliokwishakusimulia [khabari zao hapo] kabla na MItume [wengine] hatukukusimulia. Bila shaka Allaah alimzungumzisha Muusa maneno kikwelikweli.”[2]

Sisi tunawaamini Mitume wote, kuanzia wa mwanzo wao hadi wa mwisho wao, wale ambao tumetajiwa majina na wale ambao hatukutajiwa majina. Kuwaamini Mitume ni moja katika nguzo sita za imani.

أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut!”

Aayah hii ni kama ile iliotangulia:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”

Kama ambavyo Allaah amewaumba viumbe ili wamwabudu Yeye kadhalika amewatumiliza Mitume ili wamwabudu Yeye. Hakuwatuma Mitume ili wawafunze watu mambo ya kilimo na ya viwanda wala kula na kunywa. Wala hakuwatuma Mitume ili wawafanye watu wathibitishe uwepo wa Mola na uola Wake. Amewatumiliza Mitume ili wawaamrishe kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) pekee. Kwani walikubali kwamba Yeye ndiye Mola na Muumba Wao.

[1] 16:36

[2] 04:164

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 28
  • Imechapishwa: 12/08/2019