14. Kuondoka kwenda ´Arafah


61- Litapochomoza jua siku ya ´Arafah, ataondoka kwenda ´Arafah na huku analeta Talbiyah au anasema “Allaahu Akbar”. Yote hayo yamefanywa na Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hali ya kuwa walikuwa pamoja naye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika hajj yake. Yule atakayeleta Talbiyah basi afanye na asikaripiwe na yule atakayesema “Allahu Akbar” aseme na wala asikaripiwe[1].

62- Kisha atateremka Namirah[2] ambapo ni mahali karibu na ´Arafah. Hata hivyo sio katika hiyo ´Arafah. Atabaki hapo mpaka kabla ya kupinduka jua.

63- Baada ya jua kupondoka, aondoke kuelekea ´Uranah ilio karibu na ´Arafah na atashukia hapo[3]. Hapo ndipo imamu atawakhutubia watu Khutbah ambayo itanasibiana na mahali.

64- Kisha atawaswalisha watu. Dhuhr na ´Aswr zitatakiwa kufupishwa na kujumuishwa. Kadhalika zinatakiwa kuswaliwa wakati wa Dhuhr.

65- Pataadhiniwa kwa ajili ya hiyo Dhur na ´Aswr adhaana moja na Iqaamah mbili.

66- Hakuswaliwi baina yake kitu chochote[4].

67- Yule ambaye haikumuwia wepesi kuziswali hizo pamoja na imamu, basi aziswali ima peke yake au pamoja na wale walio pembezoni mwake katika watu mfano wake[5].

[1] Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

[2] Kushuka mahali hapa na kushuka kulikokuwa kabla yake kuna uwezekano isiwezekani hii leo kwa sababu ya msongamano mkubwa. Atapozifuka sehemu mbili hizo kwenda ´Arafah, hakuna neno – Allaah akitaka. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema katika “al-Fataawaa”:

“Kuhusu yale yaliyokusanywa na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kutremka kufanya ukazi katika sehemu ya Minaa siku ya Tarwiyah, kulala hapo usiku wa kuamkia siku ya ´Arafah, kufanya ukazi hapo ´Uranah – ilio kati ya mlima wa Muzdalifah na ´Arafah – mpaka wakati wa kupinduka jua, kwenda ´Arafah kwa kutokea hapo, kutoa khutbah na kuswali swalah mbili katikati ya njia ndani ya bonde la ´Uranah, ni jambo ambalo wanachuoni wameafikiana kwamba yamewekwa katika Shari´ah. Ijapokuwa waandishi wengi hawalipambanui. Vilevile watu wengi hawalijui kwa sababu ya kuzidi zile desturi zenye kuzuliwa.” (26/168)

[3] Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

[4] Kadhalika haikupokelewa kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba aliswali swalah ya sunnah kabla ya Dhuhr na baada ya ´Aswr, si hapa wala katika safari zake zote. Haikuthibiti kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali chochote katika swalah za Rawaatib isipokuwa sunnah ya Fajr na Witr.

[5] Ameipokea al-Bukhaariy kwa cheni ya wapokezi pungufu. Tazama ”Mukhtaswar al-Bukhaariy” (25/89/3).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manaasik-ul-Hajj wal-´Umrah, uk. 28
  • Imechapishwa: 15/07/2018