14. Kuoanisha kati ya ujuu na upamoja wa Allaah


Kabla hatujaanza kuoanisha sifa hizi, tunapendelea kutanguliza kanuni yenye faida ambayo Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) ameitaja katika kitabu chake ”Dar’ Ta´aarudhw-il-´Aql wan-Naql”. Kwa ufupisho ni kwamba anachomaanisha ni kuwa kukisemwa kuwa dalili mbili zinagongana, basi ima dalili zote mbili ni za kihakika au si za kihakika au moja wapo ndio ya kihakika na nyingine si ya kihakika. Kuna aina tatu:

Mosi: Dalili zote mbili za kihakika. Ina maana kwamba akili inaonelea kuwa zote mbili ni za kihakika. Katika hali hii mgongano ni jambo lisilowezekana kabisa. Kusema kuwa kuna mgongano ina maana kwamba ima moja wapo ni lazima iondoshwe, jambo ambalo haliwezekani kwa kuwa jambo la kihakika ni lazima lithibitishwe, au zote mbili zithibtishwe pamoja na kuwa zibaki ni zenye kugongana. Hili pia haliwezekani kwa sababu ni kukusanya kati ya mambo mawili yenye kugongana.

Mtu akifikiria kuwa ni zenye kugongana, basi ima si za kihakika au hakuna mgongano kati yake. Katika hali hii ina maana kwamba dalili moja inafahamika kwa njia moja na dalili ya pili kwa njia nyingine. Hivyo itakuwa maandiko ya uhakika katika Qur-aan na Sunnah hayahusiani chochote na uhakika na ufutwaji. Dalili yenye kufutwa haipo na kwa ajili hiyo hakuna mgongano uliokuja katika dalili iliyofutwa.

Pili: Hakuna dalili yoyote katika hizo mbili ambayo ni ya kihakika. Hiyo ina maana kwamba kusudio katika dalili hizo sio la kihakika au kwamba hazikuthibiti. Katika hali hii mtu anatakiwa kutafuta ile dalili yenye nguvu kisha aitangulize mbele.

Tatu: Moja katika dalili hizo iwe ni ya kihakika na nyingine isiwe ya kihakika. Katika hali hii kila mtu mwenye busara ataonelea kutanguliza mbele ile dalili yenye uhakika kwa vile yakini haiondolewi kwa dhana.

Yakibainika haya, tunasema kuwa ni jambo lisilokuwa na shaka kuwa maandiko katika Qur-aan na Sunnah yamethibitisha kuwa Allaah yuko juu ya viumbe kwa dhati Yake na kwamba yuko pamoja na wao. Sifa zote hizi mbili zimethibiti kwa uhakika na kadhalika maana yake ni ya uhakika. Allaah amezitaja zote mbili pale Aliposema:

هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۚ يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا ۖ وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ

”Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Akalingana juu ya ´Arshi. Anajua yanayoingia ardhini, na yatokayo humo, na yanayoteremka kutoka mbinguni, na yanayopanda humo – Naye Yu Pamoja nanyi popote mlipo. Na Allaah kwa myatendayo ni Mwenye kuyaona.”[1]

Katika Aayah hii Allaah (Ta´ala) anathibitisha kulingana Kwake juu ya ´Arshi Yake ambayo ndio kiumbe kilicho juu kabisa na kwamba yuko pamoja nasi. Hakuna mgongano kati ya hizo mbili. Kuna uwezekano zikaoanishwa. Zinaoanishwa ifuatavyo:

Kwanza: Maandiko yametaja yote mawili pamoja na haiwezekani kuoanishwa kwake kukawa hakuwezekani. Maandiko hayawezi kuthibitisha kitu kisichowezekana. Mwenye kudhania kwamba maana yake sio ya uhakika, amekosea na anachotakiwa ni kumuomba Allaah msaada, uongofu na mafanikio na kutafiti tena kwa umakinifu na ajitahidi kuifikia haki. Ikimbainikia haki, basi amhimidi Allaah kwa hilo. Vinginevyo amwachie suala hili yule mwenye ujuzi na aamini yale yote ambayo Allaah ameteremsha.

Pili: Hakuna mgongano kati ya ujuu na upamoja. Upamoja haulazimishi uchanganyikaji na ukitaji. Kitu kinaweza kuwa juu na kikawa na upamoja fulani. Mfano wa hilo ni kama mtu kusema:

“Hatukuacha kuwa ni wenye kusafiri na huku mwezi ukiwa pamoja na sisi.”

Mtu anaweza kusema hivi pamoja na kuwa mwezi uko mbinguni. Sentesi hii haizingatiwi kuwa ni yenye kujigonga si kilugha wala kimaana. Hapa yule mzungumzishwaji anaelewa maana ya upamoja huu na kwamba hailazimishi kuwa mwezi uko ardhini. Ikiwa ni jambo linalowezekana kwa kiumbe kukusanya kati ya ujuu na upamoja, basi kwa Muumba ni jambo la aula zaidi.

Tatu: Ikikadiriwa kuwa kuna mgongano baina ya ujuu na upamoja, basi hili ni kwa kiumbe peke yake. Haina maana kwamba haiwezekani inapokuja kwa Muumbaji. Kwa vile Allaah (Ta´ala) hakuna anayelingana Naye kwenye kitu katika sifa Zake. Kwa ajili hiyo upamoja Wake usilinganishwe na upamoja wa viumbe. Wala upamoja Wake haulazimishi kuwa ni Mwenye kuchanganyika au ni Mwenye kukita na viumbe kwa sababu Yeye ni lazima awe juu kwa dhati Yake. Isitoshe hakuna chochote katika viumbe Vyake kinachoweza kumzunguka. Bali Yeye (Subhaanah) ndiye Mwenye kukizunguka kila kitu.

Kwa njia kama hizi mtu anaweza kuoanisha kati ya ujuu uliyothibiti kwa dhati Yake na kwamba Yuko mbele ya mswalaji ifuatavyo:

Kwanza: Maandiko katika Qur-aan na Sunnah yameoanishwa kati yayo na haiwezi kuoanisha vitu viwili ambavyo ni muhali.

Pili: Kuna uwezekano kitu kikawepo mbele na wakati huo huo kikawa juu. Kwa mfano mtu anasimama mbele ya jua na jua hilo likawa liko mbinguni. Ikiwa hili linawezekana inapokuja kwa viumbe, basi inapokuja kwaMuumbaji ni aula zaidi.

Tatu: Hebu tukadirie kuwa kweli ni jambo lisilowezekana kwa kiumbe. Hata hivyo ni jambo lenye kuwezekana kwa Muumbaji. Kwa sababu hakuna chochote kinachoweza kulinganishwa na Allaah kwa njia yoyote ile. Kuwa kwake mbele ya mswalaji hailazimishi kwamba yuko sehemu au mbele ya ukuta ambao mswalaji anauelekea kwa vile Yeye ni wajibu awe juu ya viumbe kwa dhati Yake. Isitoshe hakuna chochote kiwezacho kumzunguka. Bali Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye Mwenye kukizunguka kila kitu.

[1] 57:04