14. Hoja imewasimamikia viumbe kwa Suurah “al-´Aswr”

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Lau Allaah Asingeliteremsha hoja yoyote kwa viumbe Wake isipokuwa Suurah hii, basi ingeliwatosheleza.”

MAELEZO

ash-Shaafi´iy – Ni imamu Muhammad bin Idriys ash-Shaafi´iy unasibisho wa babu yake wa nne ambaye anaitwa Shaafi´iy. Anatokana na Quraysh katika kizazi cha al-Muttwalib. Alifariki mwaka wa 204. Ni mmoja katika wale maimamu wane. Yeye ndiye amesema maneno haya. Kwa sababu ndani yake Allaah amebainisha sababu za maangamivu na sababu za kufaulu. Sababu za kufaulu ni mtu asifike kwa sifa hizi nne:

1- Elimu.

2- Matendo.

3- Ulinganizi.

4- Kuwa na subira juu ya maudhi katika njia ya Allaah (Ta´ala).

Kwa hiyo hoja ya Allaah juu ya viumbe Wake imesimama kwa Suurah hii. Allaah (Subhaanah) atawaambia kuwa aliwabainishia sababu za kufaulu katika Suurah hii fupi.

Qur-aan na Sunnah vyote ni vyenye kueleza kwa undani masuala haya mane. Lakini Suurah hii imebainisha sababu za kufaulu kwa ujumla. Matokeo yake hoja ikawa imesimama juu ya viumbe. Maandiko mengine ya Qur-aan na ya Sunnah ni yenye kuyapambanua masuala haya mane. Maneno ya ash-Shaafi´iy hayana maana kwamba endapo Allaah asingeliteremsha Suurah nyingine zaidi ya hii basi ingeliwatosha. Lakini wamesimamikiwa na hoja kwa sababu ndani yake Allaah amebainisha sababu za kufaulu na sababu za kuangamia. Hakuna yeyote atayekuja siku ya Qiyaamah na kusema kuwa hakujua sababu za kufaulu na hakujua sababu za kuangamia ilihali alikuwa akiisoma Suurah hii fupi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 36-37
  • Imechapishwa: 25/11/2020