Kinyume na hao kabisa ni wale wenye kuonelea kuwa madhehebu haya mbalimbali ni kama Shari´ah mbalimbali, kama walivoyasema hayo kwa uwazi baadhi ya wale waliokuja nyuma[1]. Wanaona kuwa ni sawa kwa muislamu kuchagua anachotaka na kuacha anachotaka – kwani yote ni Shari´ah. Huenda na hawa pia wakatumia hoja juu ya kubaki katika tofauti zao kwa Hadiyth ile batili:

“Kutofautiana kwa Ummah wangu ni rehema.”

Mara nyingi tunawasikia wakitumia hoja hiyo. Wanaipambanua kwa kusema kwamba tofauti imekuwa ni rehema kwa sababu ni kuwafanyia wasaa Ummah. Pamoja na kuwa upambanuzi wao unapingana na Aayah za wazi zilizotajwa punde kidogo na maneno ya maimamu yaliyotangulia. Ibn-ul-Qaasim amesema:

“Nimemsikia Maalik na al-Layth wakisema kuhusiana na tofauti za Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Sio kama wanavosema watu kwamba ni jambo lenye wasaa. Mambo sivyo kabisa bali hilo ni kosa.”[2]

Ashhab amesema:

“Maalik aliulizwa kuhusu mtu ambaye anapokea Hadiyth kwa mtu mwaminifu kutoka kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kama ni jambo lenye wasaa inapokuja katika kuipokea. Akajibu: “Ninaapa kwa Allaah kwamba sio hivyo mpaka pale atakapoisibu haki – na haki ni moja peke yake! Ni vipi maoni mawili yenye kutofautiana yote yatakuwa ya sawa? Haki na usawa ni mmoja peke yake.”[3]

al-Muzaniy, swahiba wa Imaam ash-Shaafi´iy amesema:

“Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walitofautiana na baadhi wakawatia wengine makosani. Baadhi wakayakagua maoni ya wengine na kuyatilia taaliki. Lau maoni yao wote yangelikuwa ya sawa basi wasingelifanya hivo. ´Umar bin al-Khattwaab alighadhibika juu ya kutofautiana kwa Ubayy bin Ka´b na Ibn Mas´uud juu ya kuswali na nguo moja. Ubayy alikuwa akionelea kuwa kufanya hivo ni jambo zuri na Ibn Mas´uud akionelea kwamba hilo lilikuwa lafaa pindi nguo zilikuwa chache. Hivyo ´Umar akatoka nje na huku amekasirika akasema: “Maswahabah wawili wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao wanatazamwa wametofautiana. Ubayy amepatia na Ibn Mas´uud hakuanguka. Lakini mimi sintomruhusu yeyote kuleta tofauti isipokuwa nitamfanya kadhaa na kadhaa.”[4]

Imaam al-Muzaniy amesema tena:

“Yule ambaye anajuzisha tofauti na anaona kwamba pindi wanachuoni wawili wana mitzamo miwili tofauti (ambapo mmoja anaona kuwa kitu fulani kinafaa na mwingine anaona kuwa hakifai) kwamba kila mmoja ni mwenye kupatia katika Ijtihaad yake, anatakiwa kuulizwa kama anasema hivo kwa sababu ya msingi au kipimo? Akisema kwamba ni kutokana na msingi, basi atambue kuwa Qur-aan inakaripia suala la tofauti – ni vipi basi itakuwa ni kutokana na msingi? Akisema kwamba ni kutokana na kipimo, basi atambue kuwa misingi inakaripia suala la tofauti – ni vipi basi utatumia kipimo juu ya misingi kwa sababu ya kujuzisha tofauti? Kitu kama hiki hakijuzishwi na mtu wa kawaida, sembuse mwanachuoni.”[5]

[1] Tazama “Faydhw-ul-Qadiyr” (1/209) ya al-Munaawiy au ”Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” (1/76-77).

[2] Ibn ´Abdil-Barr katika ”al-Jaamiy´” (2/81-82).

[3] Ibn ´Abdil-Barr katíka ”al-Jaamiy´” (2/82-83) na (2/89).

[4] Ibn ´Abdil-Barr katika ”al-Jaamiy´” (2/83-84).

[5] Ibn ´Abdil-Barr katika ”al-Jaamiy´” (2/89).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 54-56
  • Imechapishwa: 21/01/2019