14. Hadiyth “Watu hawatoacha kuwa katika kheri muda wa kuwa…. “

Hadiyth ya tisa

9- Sahl bin Sa´d as-Saa´idiy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu hawatoacha kuwa katika kheri muda wa kuwa wanaharakisha kukata swawm na wanachelewesha daku.”

Maana ya kijumla:

Shari´ah yenye hekima inasisitiza kupambanua kati ya ´ibaadah  na wakati wake kutokamana na mambo mengine ili kuweze kubainika utaratibu na utiifu katika  kutekeleza maamrisho yake na kusimama kunako mipaka yake. Kwa ajili hiyo ilipofanya kuzama kwa jua ndio wakati wa mfungaji kukata swawm ndipo ikahimiza mtu kukimbilia kufanya hivo punde tu ule wakati wa mwanzo linapozama na akaeleza kwamba watu wataendelea kuwa katika kheri midhali wanaharakisha kukata swawm. Kwa sababu mtu kwa kufanya hivo anakuwa amehifadhi Sunnah. Wakichelewesha Sunnah basi hiyo ni dalili ya wao kuondoshewe kheri  kwa sababu watakuwa wameacha Sunnah ambayo faida ya kidini ni yenye kuwarudilia wao, ambayo ni kule kufuata, na faida ya kidunia, ambayo kuichunga miili na kuifanya kuwa na nguvu kutokana na chakula na kinywaji.

 Faida zinazochukuliwa kutoka katika Hadiyth:

1- Imependekezwa kuharakisha kukata swawm watu wakiwa na uhakika kwamba jua limezama – kwa kuliona hilo – au kwa maelezo ya mtu mwaminifu.

2- Kuharakisha kukata swawm ni dalili ya kubaki kwa kheri kwa yule mwenye kufanya hivo. Kheri inakosekana kwa yule asiyefanya hivo.

3- Kheri inayokusudiwa katika Hadiyth ni kufuata Sunnah. Pamoja na kuwa ni katika mambo yanayopendwa na nafsi.

4- Hadiyth ni miongoni mwa miujiza ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwani kuchelewesha kukata swawm ni jambo linalofanywa na Shiy´ah, ambao ni moja katika makundi yaliyopotea. Hakuna wengine wanaowaiga isipokuwa ni mayahudi ambao wanafuturu wakati wa kunapochomoza nyota.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdullaah bin ´Abdir-Rahmaan al-Bassaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-´Allaam Sharh ´Umdat-il-Ahkaam, uk. (01/334-335)
  • Imechapishwa: 08/06/2018