Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah atusaidie sisi na wewe kutekeleza jukumu alilotupa na kuhifadhi Shari´ah Yake. Umeniomba kuandika kwa ufupi mambo ya wajibu ya dini ambayo yanatamkwa na ndimi, yakaitakidiwa na mioyo na kutendewa kazi na viungo vya mwili na yale mambo yaliyopendekezwa ambayo yamefungamana na mambo ya wajibu…

MAELEZO

Dini ndio jukumu lako; maamrisho na makatazo, ya halali na ya haramu. Allaah amekubebesha jukumu hilo. Allaah alizipa mbingu na ardhi na milima amana hiyo, lakini wakakataa kuibeba. Hata hivyo mwanadamu akakubali kuibeba amana hiyo. Allaah alibebesha jukumu la maamrisho na makatazo kwa mbingu, ardhi na milima wachague kama wataka. Hakuvilazimisha. Wakachagua usalama juu ya ushindi:

وَأَشْفَقْنَ مِنْهَا

“… na vikaiogopa.”[1]

Wakaogopa:

وَحَمَلَهَا الْإِنسَانُ ۖ إِنَّهُ كَانَ ظَلُومًا جَهُولًا

“… lakini mwanadamu akaibeba. Hakika yeye amekuwa dhalimu mno, mjinga mno… ”[2]

Aadam na kizazi chake wakapendelea ushindi juu ya usalama, kwa sababu mwandamu ni mjinga na dhalimu. Ndio maana akasema katika Aayah inayofuata:

لِّيُعَذِّبَ اللَّـهُ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْمُشْرِكِينَ وَالْمُشْرِكَاتِ وَيَتُوبَ اللَّـهُ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا

“… ili Allaah awaadhibu wanafiki wa kiume na wanafiki wa kike na washirikina wa kiume na washirikina wa kike na Allaah awasamehe waumini wa kiume na waumini wa kike na Allaah daima ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”[3]

Watu wamegawanyika mafungu matatu juu ya jukumu na amana hii:

1 – Wako ambao wamelibeba kwa nje na kwa ndani. Nao ni wale waumini wa kiume na waumini wa kike.

2 – Wako ambao wamelikataa kwa nje na kwa ndani. Hawa ni wale washirikina wa kiume na washirikina wa kike.

3 – Wako ambao wamelibeba kwa nje na wakalitupa kwa ndani. Hawa ni wale wanafiki wa kiume na wanafiki wa kike.

[1] 33:72

[2] 33:72

[3] 33:73

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 18
  • Imechapishwa: 06/07/2021