Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“… na kusadikisha Hadiyth juu yake.”

Bi maana Hadiyth juu ya Qadar. Kwa mfano Hadiyth ya Jibriyl:

“… na kuamini Qadar; kheri na shari yake.”

Haya ni makadirio ya jumla ambayo marejeo yake ni elimu ya Allaah yenye kuenea na ya milele na yale ambayo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ameandika kwenye Ubao uliohifadhiwa. Hadiyth ya Ibn Mas´uud inahusiana na makadirio ya umri, bi maana umri wa mwanaadamu. Katika Hadiyth yake imekuja:

“Hakika umbo la kila mmoja wenu linakusanywa  pamoja katika tumbo la mama yake kwa muda wa siku arubaini. Kisha baadaye tone la damu kwa muda kama huo. Kisha tena huwa ni kipande cha nyama kwa muda kama huo. Halafu anatumiwa Malaika ambaye anaamrishwa kuandika mambo mane; rizki yake, maisha yake, matendo yake na kama atakuwa ni mwenye furaha au mla khasara.”[1]

Haya ndio makadirio ya umri.

Vilevile kuna makadirio yenye kuitwa “makadirio ya mwaka”. Yanapangwa katika usiku wa makadirio. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ

“Hakika Sisi tumeiteremsha katika usiku uliobarikiwa – hakika Sisi daima ni Wenye kuonya [watu] – katika [usiku] huo hupambanuliwa kila jambo la hekima.”[2]

Usiku huo Allaah huandika matendo mema na maovu ya mwanaadamu, mwenye furaha au mla khasara. Makadirio yenye kupangwa katika usiku huu yanaitwa “makadirio ya mwaka”.

Pia kuna makadirio ya siku na ni yale yote ambayo Malaika wanaandika katika matendo ya mwanaadamu ya kila siku.

Imaam Ahmad amesema:

“Maswali kama “Kwa nini?” na “Vipi?” hayatakiwi kuulizwa.”

Usiulize ni kwa nini Allaah amefanya hili na kuamua lile, ni kwa nini Allaah amekataza hili na kuamrisha lile. Kinachotakiwa tu ni kuamini, kujisalimisha na kusarenda. Kwa sababu maswali kama hayo yanaweza kuwa yanatokamana na kupingana na Allaah (Tabaarak wa Ta´ala), makadirio Yake, Shari´ah Yake, makatazo na maamrisho Yake. Huna jengine zaidi ya kujisalimisha na khaswa inapohusiana na Qadar. Qadar ni siri ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Tosheka na yale unayoyajua, mengine unachotakiwa ni kujisalimisha. Usiseme “Kwa nini?” wala usiseme “Vipi?”.

Imaam Ahmad amesema:

“Kinachotakiwa ni kusadikisha na kuamini tu.”

Hili ndio la wajibu kwa kila muislamu na ndio kitu kinachohitajiwa na shahaadah; unatakiwa kujisalimisha kwa Allaah na maamrisho Yake, makatazo Yake, Shari´ah Yake na yale mazuri na mabaya ambayo Allaah amekwishakupangia.

[1] al-Bukhaariy (6549) na Muslim (2643).

[2] 44:03-04

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 376-377
  • Imechapishwa: 30/07/2017