Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Watu watapokufa watafufuliwa. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ

“Kutoka humo [ardhini] Tumekuumbeni na katika hiyo [ardhi] tutakurudisheni na kutoka humo tutakutoeni mara nyingine.”[1]

MAELEZO

Amehama kwenda katika msingi mwingine ambao ni kuamini kufufuliwa. Kwa msemo mwingine ni kwamba makusudio sio kufa peke yake. Sisi tunajua na kila mtu anajua mpaka makafiri na wakanamungu na mazanadiki kwamba ni lazima kufa. Hakuna yeyote anayepinga kifo kwa sababu ni kitu chenye kuhisiwa. Lakini shani ni kufufuliwa baada ya kufa. Hapa ndipo kwenye mgogoro kati ya waumini na makafiri. Kufufuliwa baada ya kufa ni kule kurudishwa viwiliwili vilivyoteketea na kuwa mifupa na udongo na kutawanyika ardhini vitarudishwa na kuwa kama vilivyokuwa hapo kabla. Kwa sababu ambaye kaweza kuvikuza hapo mara ya kwanza ni muweza wa kuvirudisha. Baada ya hapo vitapuliziwa roho na vitatikisika na vitatembea kutoka ndani ya makaburi na kwenda katika uwanja wa mkusanyiko. Amesema (Ta´ala):

يَوْمَ يَخْرُجُونَ مِنَ الْأَجْدَاثِ سِرَاعًا كَأَنَّهُمْ إِلَىٰ نُصُبٍ يُوفِضُونَ

”Siku watapotoka makaburini upesiupesi kama kwamba wanakimbilia golini.”[2]

خُشَّعًا أَبْصَارُهُمْ يَخْرُجُونَ مِنَ الْأَجْدَاثِ كَأَنَّهُمْ جَرَادٌ مُّنتَشِرٌ مُّهْطِعِينَ إِلَى الدَّاعِ

”Macho yao yakiwa dhalili, watatoka makaburini kama kwamba wao ni nzige waliotawanyika; wenye kukimbia mbio huku wakibenua shingo zao wakielekea kwa mwitaji.”[3]

Hakuna hata mmoja atakayebaki nyuma. Huku ndio kufufuliwa kusikokuwa na shaka. Mwenye kupinga jambo hilo ni kafiri.

Kuamini kufufuliwa ni moja katika nguzo sita za imani ambazo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yake:

“Kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, siku ya Mwisho na kuamini Qadar kheri na shari yake.”

 Asiyeamini kufufuliwa na siku ya Mwisho anakuwa kafiri ambaye amemkufuru Allaah (´Azza wa Jall). Haijalishi kitu hata kama anashahuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah ingawa ataswali, atahiji, atatoa zakaah na akafanya matendo mema. Akipinga kufufuliwa na akatilia shaka basi anakuwa kafiri mwenye kumkufuru Allaah (´Azza wa Jall). Dalili za kufufuliwa ni nyingi ikiwa ni pamoja na maneno Yake (Ta´ala):

مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ

“Kutoka humo [ardhini] Tumekuumbeni… “

Bi maana ardhi ambayo aliumbwa Aadam (´alayhis-Salaam) ambaye ndiye baba wa watu:

وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ

“… na katika hiyo [ardhi] tutakurudisheni.”

Bi maana baada ya kufa kutoka ndani ya makaburi:

وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ

“… na kutoka humo tutakutoeni mara nyingine.”

Huku ndio kufufuliwa. Aayah hii ndani yake kuna kuanzishwa na kurudishwa:

مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ

“Kutoka humo [ardhini] Tumekuumbeni na katika hiyo [ardhi] tutakurudisheni na kutoka humo tutakutoeni mara nyingine.”

[1] 20:55

[2] 70:43

[3] 54:07-08

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 276-278
  • Imechapishwa: 16/02/2021